Madhara Ya Mtazamo
Madhara chanya na hasi ya mtazamo
Ikiwa unataka kufanikiwa katika eneo lolote maishani mwako unapaswa kwanza kujifunza namna ya kufikiri vizuri,kwa sababu pengo kati ya watu waliofanikiwa na wale ambao hawajafanikiwa,lipo katika namna wanavyofikiri (mtazamo)
Mwalimu na mhubiri John Maxwell anasema “kama unataka kuwa mtu mwenye mafanikio kwako na watu wengine lazima ujenga mfumo fulani wa kufikiri na mtazamo utakaobadilisha unavyojiona na namna unavyoiona dunia”
Hauhitaji kuwa na degree,kuwa mrefu wala mfupi,wala huhitaji kuwa mwembamba wala mnene,wala huhitaji kutoka katika nchi fulani hapana hata kama utakuwa ni mtu mwenye akili sana kama mtazamo wako ni mdogo hutaweza kufaulu kufanikiwa katika jambo lolote.
Kila kitu unachoona leo vikubwa na vidogo,vinavyokushangaza na vile usivyoshangaa ni matokeo ya watu kufikiri,tangu zamani watu walikuwa wanafikiri,hata sasa watu wanafikiri na wataendelea kufikiri siku zote. Lakini kufikiri siyo jambo muhimu ila namna mtu unavyofikiri ndicho kitu kinachoathiri mambo mengi katika dunia hii tunayoishi.
Watu wanakwama katika mambo mengi wanayofanya pale wanapokutana na matatizo yoyote ambayo yanasababisha safari yao kususua,matokeo yake wanajikuta kushindwa kufanya kile walichokusudia kwa kuheshimu kile wanachoita matatizo.
Kila mtu anazo changamoto katika maisha kwani hiyo ni sehemu ya mchakato wa kuishi lakini wakati watu wasiofikiri vizuri wanaita matatizo, matatizo,watu wanofikiri vizuri wao wanaita changamoto kwani kinywani mwao hakuna nano matatizo.
Kwa kubadili tatizo kuwa katika sura ya changamoto inawapa nafasi ya kutafuta njia ili kupita kwenye hiyo changamoto. Kwa nini? Kwa sababu tatizo husukuma akili kufikiri kuwa ni mlima mrefu ambao ni mgumu kuupanda, lakini tatizo hilo hilo ukilibadili na kuliweka katika sura ya changamoto ni kitu cha msimu kinachowezekana kukivuka.
Changamoto huja kwa msimu na kwa kawaida changamoto haipaswi kuwa kitu cha kudumu.Mtu anayefikiri vizuri yeye huitazama changamoto kama kizuizi ambacho nyuma yake kuna fursa kubwa kwa hiyo hawezi kutulia mpaka amepata majibu ya changmoto hiyo.
Jambo muhimu kujua ni kwamba Mungu hawezi kukuletea changamoto ambayo haina faida katika maisha yako,lazima ukipita changamoto utajikuta umevuka kutoka hatua moja chini kwenda juu ambapo hungeweza kufika bila kupitia changamoto.
Huwezi kupanda juu bila kuwepo na utaratibu wa kukuwezesha kupanda juu kwa urahisi hivyo wanaofikiri vizuri changamoto kwao huwa ni kama ngazi ya kuwapandisha kutoka sehemu moja kwenda juu.
Je wewe ni miongoni mwa watu waliokwama kutokana na jinsi unavyofikiri na pengine umeshindwa kufanya kitu chochote kutokana tu na jinsi unavyojiona na unavyoiona dunia? Nataka nikukumbushe tu kwamba kufanikiwa au kutokufanikiwa kuko mikononi mwako kama utaweza kutabadili tu unavyofikiri.
Kama kazi yako ni kuwaza jinsi ambavyo kila kitu unachotaka kufanya hakiwezekani kwa sababu kwenu hajawahi kutokea mtu kufanya kitu kama hicho hutafanikiwa mpaka utakapobadili jinsi unavyoona moyoni mwako.
Iwapo kila siku unataka kufanya jambo fulani iwe ni biashara au ni kazi yoyote ambayo unajua kabisa moyoni mwako kwamba ingeleta manufaa makubwa kwako na jamii unashindwa kwa sababu tu unajiona wewe ni mtu usiye na uwezo,basi hivyo ndivyo ulivyo huwezi kufanya kitu chochote cha ajabu mpaka hapo tu utakapobadili hiyo imani.
Kumbuka mtazamo hutokana na imani,na kama mtazamo ni tunda la imani basi huwezi kuwa na mtazamo zaidi ya imani yako haiwezekani.Unataka kubadilika haraka lazima ubadili unavyoamini na kuathiri unavyofikiri.
Wazazi wetu na mfumo umetufundisha kuwa ni muhimu kwenda shule ili tupate kazi nzuri na hakuna anayekuambia usome ili ufanye biashara na kuajiri watu wengine.Wala hakuna anayekuambia kuwa usome ili uje kuwa na kazi binafsi ambayo wewe mwenyewe utakukuwa mwajiri.
NAMNA YA KUFIKIRI
Hakuna mtu anaweza kuishi zaidi ya anavyofikiri na kujiona ndani mwake,kwa hiyo kama unataka kubadili unavyoishi sasa unapaswa kubadili mfumo wa jinsi unavyoamini.Maisha yako ni matokeo ya unavyofikiri,hivyo ndivyo ilivyo. Umeumbwa kufanya kitu cha pekee hapa duniani hukuja kwa bahati mbaya na unapaswa kuamini hivyo. Wewe ni ni wa pekee. Kama ambavyo mtu mmoja na mwingine hatufanani sura basi ndivyo ilivyo hata kwa habari ya vipaji mbalimbali tulivyobeba ndani mwetu.
Watu wote waliowahi kuishi na wale ambao bado tunaishi tumegawanyika katika makundi mawili.Kundi la wale wakifa wanakufa kabisa na kundi la wale watu ambao watakuendelea kuishi hata kama watakapokuwa wamekufa. Kinachowatofautisha watu katika makundi haya mawili siyo walivyoishi,bali katika maisha yao waliigusa dunia kwa namna gani ndicho kitu kikubwa kinacholeta tofauti kubwa katika maisha ya watu kwenye makundi hayo mawili.
Je wewe unajiona kama mtu mdogo usiyeweza kufanya chochocte na kujihukumu kutokana na historia? Fanya mabadiliko jinfunze kufikiri vizuri kwani uonavyo moyoni mwako ndivyo ulivyo na huwezi kuishi zaidi ya unavyoamini.
Ni mimi rafiki na kocha wako: Philipo Lulale
WhatsApp: +255784503076
Barua Pepe: maishanifursa2017@gmail.com