Usidharau Mwanzo Mdogo

Usidharau mwanzo mdogo

Kila kazi au biashara unayotaka kufanya ni muhimu kukumbuka kwamba unahitajika angalau uwe na maarifa ya msingi ya kukuwezesha kufanya biashara hiyo.Maarifa hayo yanaweza kuwa umeyapata kutoka shuleni au hata kutokana na uzoefu wa muda fulani ukifanya au ukimsaidia mtu.Maarifa yanakuwezesha kujua mazuri na mabaya yaliyo ndani ya fursa hiyo ya kufuga kuku.Kipengenere hicho ukikiruka unaweza ukapata hasara kwanza kabla ya kuingia kupata faida.

Kama unataka kuwa mmiliki na mfanya biashara mkubwa wa shamba la kuku.Ukija kwangu nitakushauri kuwa anza kidogo kidogo kuuza mayai. Utaanza kwa kuuza mayai uliyonunua kutoka kwa watu ambao tayari wanafuga. Utawekeza fedha kiasi kununua mayai kutoka kwa wafugaji ambao tayari wanafuga kuku,na kuyauza kwa walaji.Uza,uza,uza na kuuza Zaidi na Zaidi na kadri utakavyouza utajikuta unajifunza mambo mengi kuhusiana na biashara ya ufugaji kuku ambayo kabla hukuyajua.

Utaona kwa kuanzia pale ulipo na kufanya kile unachoweza kufanya,umeanza safari yako ya kuelekea kufanya unachotaka kwa kumiliki biashara kubwa ya shamba la kuku na itakuwa rahisi kwani umekwisha anza tayari kupitia kwenye njia ya maono yako.

Sijui kama unajua tofauti kati ya kufanya unachoweza kufanya na kufanya unachotaka kufanya. Kufanya unachoweza ni pale unapaswa kufanya kile kilichopo ndani ya uwezo wako hata kama siyo kama unavyotamani kufanya.Na kufanya unachotaka ni kufanya kile unachotaka bila kuwepo na kizuizi cha aina yoyote.

Watu wengi wanaanza kufanya wanachoweza kufanya kabla ya kuanza kufanya wanachotaka.Na watu wengi wanakwama kwa kurukia kufanya wanachotaka kabla ya kuanza kufanya wanachoweza.Kuna somo kubwa wanaliruka na mwisho inaweza kumgharimu mtu muda na fedha nyingi kurudi kwenye njia.

Katika safari hiyo ya kuvutia utagundua kuwa,licha ya kufanya biashara kuna mambo mengi sana muhimu utakuwa unajifunza njiani ambayo kabla ya kuanza ulikuwa huyajui kabisa.Utawajua wafugaji wakubwa na wadogo wa kuku wa nyama na hata mayai.Utapata wateja wa mayai,wakubwa na wadogo na pesa yako itakua kutokana na faida unayotengeneza kwa kuuza mayai.Vile vile utajifunza changamoto nyingi kwenye biashara hiyo.

Mahusiano mengine yatakayotengenezwa na biashara yako hiyo utajenga uaminifu kwa wafugaji ambao wewe ni mteja wao na kwa wanunuzi ambao wao ni wateja wako,wote watakuwa wanakutegemea. Haitashangaza siku nyingine wafugaji kukukopesha mzigo mkubwa wa mayai tofauti na mtaji wako ukiuza unalipa pesa. Bila kuanza hakuna mtu angekuamini na kukukopesha mayai.

Utaanza kuaminiwa na vyombo vya fedha na wengine kuanza kukushauri namna unavyoweza kupanua biashara yako kwa kukopa mtaji mkubwa benki,ambazo ziko tayari kukuamini na kukukopesha kiasi cha pesa ambayo ungehitaji kwa kuwa umeonyesha uwezo mkubwa wa kuendesha biashara kwa mafanikio. Ziko faida nyingi lakini nyingine ni watu wenye mtaji mkubwa wa fedha (wawekezaji) watajenga imani kwako kiasi cha kuweza hata kuweka mikono na fedha zao kwenye kile unachokifanya utakapohitaji.

Mtu aliyefika hatua hiyo sasa nitamshauri kuwa anaweza kuanzisha biashara yake ya shamba kubwa la kuku kwa kuwa ana kila anachohitaji mtu kuwa nacho ili kufanikiwa katika biashara ya kuendesha shamba kubwa la kuku wa mayai na nyama.Soko analijua na changamoto ana taarifa nazo. 

Ana uzoefu wa kutosha na maarifa ya kutosha ya namna ya kuendesha biashara hiyo na taarifa muhimu za namna ya kufanikiwa katika biashara hiyo,zikiwemo zile zinazoitwa changamoto katika biashara ya ufugaji wa kuku na hakuna cha kuweza kumsimamisha mtu huyu anayepita kwenye ndoto yake. Kwa kifupi ana uzoefu wa kutosha.

Maisha ni fursa bila mipaka na hakuna kitu cha kuweza kukuzuia kuwa chochote unachotaka kuwa hapa duniani. Kama kuna kitu unafikiri kufanya lakini unakwama kwa kile unachosema kukosa mtaji,nakushauri uanzie pale unapoweza kufanya kama njia sahihi ya kuelekea kufanya unachotaka kufanya.

Naamini kuna kitu umepata katika makala hii fupi.Kama utakuwa na uhitaji wa ushauri wa namna ya kuboresha katika eneo lolote la maisha,au ungependa kuingia ndani Zaidi ya somo hili unaweza kuwasiliana nami kwa whatsapp,ujumbe mfupi wa maneno,au hata kupiga simu hapo chini.
Ni mimi rafiki na kocha wako: Philipo Lulale
WhatsApp: +255784503076
Barua Pepe: maishanifursa2017@gmail.com

Previous
Previous

Jifunze Kusema Hapana Itakusaidia…

Next
Next

Madhara Ya Mtazamo