Safari ya Ndoto: Dr. Kakenya Anayeishi Maono Yake.

DR. KAKENYA ALIKUBALI KUKEKETWA KWA SHARTI LA KUTIMIA NDOTO YAKE YA KUPELEKWA SHULE. (Picha kwa hisani ya mtandao)

Miongoni mwa visa vya kusisimua vya hivi karibuni kutokea katika bara la Afrika na dunia kwa ujumla ni kisa cha msichana wa kimasai wakati huo ambaye alikubali kukeketwa kwa sharti la kurudi shule baada ya kukeketwa badala ya kuoelewa kama ilivyokuwa desturi ya wamasai. Katika simulizi hii ambayo  Kakenya Ntaiya anasimulia mwenyewe utabaini jinsi msichana huyu raia wa Kenya alivyoweza kubadilisha uzoefu na uchungu wa kukeketwa kuwa ndoto kubwa ya kubadilisha maisha ya mabinti wengi wa kimasai.

"Naitwa Kakenya Ntaiya. Nilizaliwa katika kijiji kidogo kusini magharibi mwa Kenya. Hakukuwa na umeme,maji safi wala barabara nzuri wakati huo.Kumbukumbu zangu za utotoni ni kuchunga ng’ombe na kwenda kuchota maji. Kuogesha wadogo zangu na kuwapikia chakula. Katika kabila la wamasai wanawake hawapumziki ni kwenda kwenda kwenda tu.

Tulikuwa hatukai na baba yetu nakumbuka alikuwa anaweza kuja nyumbani kama mara moja kwa mwaka na uzoefu wangu na baba ulikuwa mgumu sana kutokana na alivyokuwa anamfanyia mama matendo ya kikatiri na kumpiga mara kwa mara haiku uzoefu mwepesi hata kidogo maana hakutujali kabisa. Kuwa msichana au mwanamke katika utamaduni wa kabila langu ilikuwa ni lazima kukeketwa. Wanakukeketa kwa njia za kiasili bila hata tahadhari yoyote ya kiafya.

Katika kabila la wamasai wavulana huandaliwa kuwa mashujaa na wasichana huandaliwa kuwa mama wa nyumbani. Nilipotimiza umri wa miaka 5 nilibaini kwamba kumbe nilikuwa nategemewa kuozeshwa muda mfupi tu baada ya kuvunja ungo. Mama yangu,shangazi zangu na bibi zangu wote mara kwa mara walinikumbusha kuwa nina mume wangu mara tu baada ya kuvunja ungo. Chochote kilichokuwa kinafanywa kwangu ilikuwa ni kuniandaa kuwa mwanamke bora nitakapofikisha umri wa miaka 12. Kila siku niliamka saa 11 alfajiri kukamua maziwa,kupikia wadogo zangu chakula,kukusanya kuni,kuteka maji,nilifanya kila nilichotakiwa kufanya kuwa mwanamke kamili.

Nilienda shule si kwa sababu wasichana wa kimasai huenda shule kwa sababu mama yangu alinyimwa fursa ya elimu na siku zote mimi na wadogo zangu alitukumbusha kuwa kamwe hangetamani tuishi maisha aliyoishi yeye;kwa nini alisama hivyo? Baba yangu alikuwa anafanya kazi kama polisi huko mjini alikuja nyumbani mara moja kwa mwaka. Hatukumwona hata wakati mwingine zaidi ya miaka miwili. Wakati alipokuja nyumbani ilikuwa ni shughuli nyingine: mama yangu alifanya kazi ngumu za kulima ili kupata chakula ambacho tungekula.alifuga ng’ombe na mbuzi ili aweze kututunza. Lakini baba yetu alipokuja aliuza ng’ombe,aliuza mazao yetu na kwenda kunywa pombe na marafiki zake,kwa sababu mama yangu alikuwa mwanamke hakuruhusiwa kumiliki mali yoyote. Na kama mama akimuuliza alimkejeli na kumpiga kwa kweli ilikuwa ngumu sana.

Nilipokwenda shule nilikuwa na ndoto “nataka kuwa mwalimu’ nilipenda waalimu jinsi walivyokuwa wanavaa,na mwonekano wao ulinivutia sana. Nilifikiri kazi ya waalimu ilikuwa ni kuandika tu kwenye ubao kazi ambayo haikuwa ngumu kama niliyokuwa nafanya shambani. Nilisoma kwa bidii sana na nilipofikia darasa la nane ilikuwa ni dhamira yangu kuendelea ili nie mwalimu. katika kabila letu kuna sherehe ambayo mwanamke lazima afanyiwe ili kukamilika kama mwanamke. Kipindi hicho nilikuwa natakiwa kujiunga na elimi ya sekondari lakini wakati huo huo niliona ndoto yangu ya kuwa mwalimu ilikuwa inafika ukingoni maani ilikuwa ni lazima nikeketwe ili kukamilika kuwa mwanamke bora wa kimasai.

Kwa hiyo niliongea na baba yangu na kufanya kitu ambacho wasichana wengi hawakuwahi kufanya. Nilimwambia baba yangu nitakubali kukeketwa endapo tu angeniruhusu kurudi shule baada ya sherehe. Ilibidi nifanye hivyo kwa sababu kama ningekimbia baba yangu angepitia kipindi cha unyanyapaa mkubwa maana jamii ingesema huyu ndiye baba wa binti aliyekata kupitia mila ya kukeketwa. Ilikuwa ni kitu cha aibu sana kama ingetokea nikakimbia kufanyiwa sherehe. Kwa hiyo baba yangu alinikubalia kuwa utaenda shuleni baada ya sherehe ya kukeketwa. Nilikeketwa na kuvuja damu nyingi sana baada ya hapo nilizimia. Ni hatua ambayo watu wengi hupoteza maisha nina bahati lakini wengi hupoteza maisha. Nilkuwa na bahati kwa sababu mama yangu alifanya kitu ambacho kina mama wengi walikuwa hawafanyi.Baada ya kukeketwa alimtafuta muuguzi ambaye alituhudumia vizuri na baada ya wiki tatu tulipona. Nilikuwa na dhamira kuu sasa kuwa mwalimu ili niweze kusababisha mabadiliko katika jamii yangu.

Baada ya kurudi shuleni kuna kitu kilitokea. Nilikutana na kijana aliyekuwa anatoka katika chuo kikuu cha Origan nchini Marekani hiki kitu kilinivutia sana. Huyu kijana alivaa tisheti nyeupe,jeans na mkononi alishika kamera na alivaa viatu. Alinivutia sana. Nilimwambia nataka kwenda huko aliko kwa sababu alionekana kuwa mwenye furaha na nilimshangaa sana. Aliniuliza una maana gani huna mume mtarajiwa anaekusubiri? Nilimwambia usijali kuhusu hiyo niambie tu namna ya kwenda uliko wewe. Huyu mtu alinisaidia sana na nilipokuwa shule baba yangu aliumwa alipooza kwa hiyo alikuwa anaumwa kweli na hakuweza tena kuniambia nini cha kufanya baadaye.

Lakini tatizo lilikuwa yeye hakuwa ni baba yangu pekee yake maana katika kabila letu mtu yeyote wa rika la baba yangu alikuwa ni baba na aliweza kuniamulia vyovyote kama baba yangu,wajomba zangu waliweza kuamua kesho yangu itakavuyokuwa. Kwa hiyo niliomba nafasi ya chuo na kukubrliwa kaujiunga na chuo cha wanawake cha “Random Macon women college huko Lynchburg Virginia niching Marekani. Nilipata ufadhili lakini ilikuwa ni lazima nitafute pesa kwa ajili ya mahitaji ya ticket na mengineyo kwa hiyo nilihitaji msaada kutoka kwa jamii yangu. Tatizo lilitokea tena maana wanaume waliposikia kuna mwanamke anataka kwenda kusoma nje ya nchi walichukulia kama ni fursa iliyopotea kwa sababu hiyo ingekuwa imetolewa kwa mvulana hatuwezi walikata kuwa hawawezi kusomesha mtoto wa kike. 

Mimi sikukata tamaa nilifanya kitu na kuendelea kupambana. Katika mila za kimasai kuna imani kwamba siku njema huanza asubuhi kwa hiyo niliamka asubuhi na mapema na kwenda kwa mzee wa kimasai ambaye anaheshimika sana.Kwa utaratibu wa kimasai kuna mee mmoja ambaye anaheshimika sana krasi kwamba akisema jambo huyo hakuna mtu anaeweza kumbishia na huyu ndiye niliyemwendea. Aliponiona aliniuliza mwanangu kwa nini uko hapa asubuhi na mapema hivi? Nilimwamnbia nahitaji msaada wake na nilimwamjulisha kuwa nataka kwenda Marekani kusoma nimepata ufadhili,niliahidi kuwa nitarudi kuitumikifa jamii yangu ya kimasai nikimaliza chuo na ningekuwa mwanamke bora katika jamii ambaye atafanya chochote ambacho wangetaka nifanye. Ingawa alikubali kunisaidia lakini aliniambia kuwa hangeweza peke yake kwa hiyo aliniunganisha na wazee wengine 15 ambao nilienda kwao kila siku asubuhi na mapema moja baada ya mwingine kuomba msaada wao.Nilifanikiwa kupata pesa ya kutosha na kuanza safari yangu mpya ya masomo Marekani.

Baada ya kufika Amerika na kuanza masomo nilifurahia sana maisha huko. Hata hivyo baada ya muda nilikuja kujifunza kwamba kile kitendo nilichofanyiwa nikiwa na umri wa miaka 13 ilikuwa ni kinyume cha Sheria za Kenya na haki za binadamu. Nilijifunza kwamba sikupaswa kuuza sehemu ya mwili wangu kwa ajilli ya elimu. Nilijifunza kumbe ilikuwa ni ukeketaji. Na sasa hivi ninavyoongea wasichana zaidi ya milioni 3 barani Afrika wako katika hatari ya kukeketwa. Nilijifunza kwamba mama yangu pia alikuwa na haki ya kumiliki mali na hakupaswa kabisa kudhalilishwa kwa namna yoyote ile kwa sababu tu ni mwanamke. Mambo hayo yote yalinifanye niwe na hasira kwa hiyo nilidhamiria kuwa nilihitaji kufanya kitu.

Kila niliporudi nyumbani likizo nilishughudia wasichana wadogo wa kimasai wakilazimishwa kuolewa na watu ambao hawakuwapenda tena kabla ya kutimiza ndoto zao maishani. Baada ya kuhitimu chuo kikuu nilirudi nyumbani na hapo kilio cha mabinti wa kimasai waliokuwa wanapitia uzoefu ambao mimi nimepitia iligeuka kuwa mzigo mkubwa kwangu na hapo niliamua kwamba lazima nifanye kitu.

Nilirudi nyumbani na kuanza kuzungumza na wanawake na wanaume kuwauliza ni nini wangependa niwafanyie kama nilivyoahidi? Wanawake waliniambia kuwa haijawahi kuwepo shule kwa ajili ya wasichana wa kimasai katika jamii hiyo. Kwa nini walitaka shule kwa ajili ya watoto wa kike wa kimasai ni kwa sababu msichana alipobakwa wakati anakwenda shule lawama ilimrudia mama endapo binti angepata ujauzito. Ni aibu kwa mama ataadhibiwa na kupigwa kwa kitendo cha msichana kupata mimba kabla ya kuolewa bila kujalisha kwamba alibakwa.

Nilipozungumza na kina baba unaweza kuhisi walisemaje. Walisema wanataka shule kwa ajili ya wavulana. Niliwaambia Sawa lakini kuna shule nyingi kwa ajili ya wavulana na wavulana Wengi wamepata fursa ya kusoma hata nje ya nchi,niliwashawishi kwa nini tusijenge shule ya wasichana kwanza halafu tutajenga shule ya wavulana? Walikubaliana nami. Lakini niliwaambia nataka kuaona dhamira ya kweli kutoka kwao kuwa wanataka kuwa na shule kwa ajili ya wasichana. Kwa kweli waliwajibika na kunipatia ardhi bure mahali ambapo leo imejengwa shule ya wasichana wa kimasai ambayo imeleta mageuzi makubwa katika mila za kimsai kwe nye jamii.   

Tulianza na darasa moja la wanafunzi 30 na kila mwaka tulikuwa tunaongeza darasa moja la wanafunzi 40. Sasa hivi tunaelimisha zaidi ya wasichana 200 kila mwaka na tayari tuna wasichana wa kimasai wahitimu wa vyuo vikuu mbalimbali katika nchi yetu na kazi inaendelea”

Lengo la kukuwekea simulizi hii ambayo Kakenya mwenyewe amejieleza kwa nia ya mtandao wa youtube alipokuwa anatoa ushuhuda huko nchini Marekani katika jukwa la wanenaji maarufu la TED TALKS ni kukusaiadia msomaji wangu ujifunze kitu kuwa wakati mwingine tumekosa fursa muhimu na kusababisha mabadiliko katika maisha na jamie kwa ujumla kwa kutokujua tu kwamba matatizo ni ngazi muhimu sana kutusaidia kuishi ndoto zetu kubwa katika maisha. Kakenya alibadilisha uchunhgu wake kuwa huduma ambayo imebeba maono na matokeo makubwa katika jamii yake ya kimasai.

Naamini utakuwa umepata kitu kupitia makala hii fupi. Ukiwa na uhitaji wowote au ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasiliana nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini.

Unapitia jambo lolote gumu na kujiona kana kwamba mwisho wa kila kitu umefika huwezi kufanya jambo lolote? wasiliana nasi tukusaidie uanze kuamka na kuishi maisha ya kusudi la kuwepo kwako hapa duniani.

Previous
Previous

“Nguvu Ya Imani Katika Kila Unalofanya”

Next
Next

Huwezi Kuvuna Usichopanda.