Anzia Pale Unapoweza.

Uzuri wa kuanzia unapoweza

Kuna tofauti kati ya kufanya unachoweza kufanya na kufanya unachotaka kufanya. Kufanya unachoweza ni pale unapopaswa kufanya kile kilichopo ndani ya uwezo wako hata kama siyo kama unavyotamani kufanya.Na kufanya unachotaka ni kufanya kile unachotaka bila kuwepo na kizuizi cha aina yoyote.Watu wengi wanaanza kufanya wanachoweza kufanya kabla ya kuanza kufanya wanachotaka.  

Makala yangu ya leo natamani kukumbusha jambo muhimu sana ambalo mtu anayetaka kufanikiwa akilifuatailia atafika anakotaka kufika na mwisho wa siku kuwa mfano wa kuigwa na watu wote wanaotamani kufanikiwa. Fulani ana bahati kweli,ana miradi mikubwa inayomwingizia pesa nyingi,lo watu wengine walizaliwa na bahati! Fulani hana bahati ila ana juhudi na anajua anachofanya,kwa hiyo anajua anakotoka,aliko na anakotakiwa kwenda.Hicho ndicho watu wengi hawana. 

TOFAUTI KATI YA WANAOFANIKIWA NA WALE WASIOFANIKIWA.

Tofauti kati ya watu wanaofanikiwa na wale wasiofanikiwa haiko kwenye bahati waliyonayo, ila iko kwenye maono,taarifa na juhudi. Watu wanaotafuta na kufanikiwa utakuta wanafanikiwa katika kila jambo ambalo wataweka mikono yao,na hakuna kitu cha kuweza kuwasimamisha. Kitu cha kwanza walichobeba ndani mwao bila kujali hali yao kifedha wana maono na kupitia maono hayo wanayo picha ya mahali wanakota kwenda na chochote watakachokuwa wanafanya sasa ni mazoezi ambayo yatawawezesha kufika kule wanakotaka kufika.

Jambo la pili walilo nalo wana taarifa juu ya kile kinachoendelea katika ulimwengu wao wa ndani na kinachoendelea katika ulimwengu wa nje.Kwa kuwa na taarifa wanajua gharama watakayoingia mpaka kufika kule wanakotaka kufika.Wanajua watahitaji kutumia muda na wanaishi kama wao bila kuiga mtindo na mfumo wa maisha wa mtu mwingine.  

Kitu cha tatu walichonacho ambacho ni muhimu kuwa nacho ni juhudi ya kufanya kile unachojua ambacho kimekupa maono.Sasa kila atakachofanya kitakuwa kinamsaidia kuifikia ile hatma aliyojiwekea kuifikia.Atafanya,atafanya,atafanya bila kuchoka na mwisho wa siku atafika anakokwenda.

Watu wengi wenye ndoto ambazo hazijatekelezwa ukiwauliza kwa nini hawafanyi kile wanachoota watakwambia kuwa hawana fedha.Hebu angalia kama kuna mahali mimi nimeitaja pesa hapo juu.Sina maana pesa haina umuhimu katika safari ya mafanikio hapana tunachotofautiana ni kwamba hatuanzi na pesa kwa kuwa vipo vichocheo vingi vya maanikio kabla ya kuhitaji pesa. Ujumbe ninaotaka kuuachilia leo ni kwamba tunapaswa kuanza kidogo kidogo hasa kuanzia pale tulipo.Hebu tutumie mfano wa mtu huyu anayetaka kuwa mfanya biashara mkubwa wa shamba la kuku wa nyama na mayai.

UMUHIMU WA KUANZIA UNAPOWEZA….

Kama unataka kuwa mmiliki na mfanya biashara mkubwa wa shamba la kuku.Ukija kwangu nitakushauri kuwa anza kidogo kidogo kuuza mayai. Utaanza kwa kuuza mayai uliyonunua kutoka kwa watu ambao tayari wanafuga. Utawekeza fedha kiasi kununua mayai kutoka kwa wafugaji ambao tayari wanafuga kuku,na kuyauza kwa walaji.Uza,uza,uza na kuuza Zaidi na Zaidi na kadri utakavyouza utajikuta unajifunza mambo mengi kuhisiana na biashara ya ufugaji kuku ambayo kabla hukuyajua. Utaona kwa kuanzia pale ulipo na kufanya kile unachoweza kufanya,umeanza safari yako ya kuelekea kufanya unachotaka kwa kumiliki biashara kubwa ya shamba la kuku na itakuwa rahisi kwani umekwisha anza tayari kupitia kwenye njia ya maono yako.

Sijui kama unajua tofauti kati ya kufanya unachoweza kufanya na kufanya unachotaka kufanya. Kufanya unachoweza ni pale unapswa kufanya kile kilichopo ndani ya uwezo wako hata kama siyo kama unavyotamani kufanya.Na kufanya unachotaka ni kufanya kile unachotaka bila kuwepo na kizuizi cha aina yoyote. Watu wengi wanaanza kufanya wanachoweza kufanya kabla ya kuanza kufanya wanachotaka.Na watu wengi wanakwama kwa kurukia kufanya wanachotaka kabla ya kuanza kufanya wanachoweza.Kuna somo kubwa wanaliruka na mwisho inaweza kumgharimu mtu muda na fedha nyingi.

MASOMO MUHIMU KWA KUANZA KIDOGO KIDOGO

Katika safari hiyo ya kuvutia utagundua kuwa,licha ya kufanya biashara kuna mambo mengi sana muhimu utakuwa unajifunza njiani.Utawajua wafugaji wakubwa na wadogo wa kuku wa nyama na hata mayai.Utapata wateja wa mayai,wakubwa na wadogo na pesa yako itakua kutokana na faida unayotengeneza kwa kuuza mayai. Mahusiano mengine yatakayotengenezwa na biashara yako hiyo utajenga uaminifu kwa wafugaji ambao wewe ni mteja wao na kwa wanunuzi ambao wao ni wateja wako,wote watakuwa wanakutegemea. Haitashangaza siku nyingine wafugaji kukukopesha mzigo mkubwa wa mayai tofauti na mtaji wako ukiuza unalipa pesa. Bila kuanza hakuna mtu angekuamini na kukukopesha mayai.

Utaanza kuaminiwa na vyombo vya fedha na wengine kuanza kukushauri namna unavyoweza kupanua biashara yako kwa kukopa mtaji mkubwa benki,ambazo ziko tayari kukuamini na kukukopesha kiasi cha pesa ambayo ungehitaji kwa kuwa umeonyesha uwezo mkubwa wa kuendesha biashara kwa mafanikio. Ziko faida nyingi lakini nyingine ni watu wenye mtaji mkubwa wa fedha (wawekezaji) watajenga imani kwako kiasi cha kuweza hata kuweka mikono na fedha zao kwenye kile unachokifanya utakapohitaji. Mtu aliyefika hatua hiyo sasa nitamshauri kuwa anaweza kuanzisha biashara yake ya shamba kubwa la kuku kwa kuwa ana kila anachohitaji mtu kuwa nacho ili kufanikiwa katika biashara ya kuendesha shamba kubwa la kuku wa mayai na nyama.Soko analijua na changamoto ana taarifa nazo. 

Ana uzoefu na maarifa ya kutosha ya namna ya kuendesha biashara hiyo na taarifa muhimu za namna ya kufanikiwa katika biashara hiyo,zikiwemo zile zinazoitwa changamoto katika biashara ya ufugaji wa kuku na hakuna cha kuweza kumsimamisha mtu huyu anayepita kwenye ndoto yake.  

Maisha ni fursa bila mipaka na hakuna kitu cha kuweza kukuzuia kuwa chochote unachotaka kuwa hapa duniani. Kama kuna kitu unafikiri kufanya lakini unakwama kwa kile unachosema kukosa mtaji,nakushauri uanzie pale unapoweza kufanya kama njia sahihi ya kuelekea kufanya unachotaka kufanya.

Previous
Previous

Funguo Sahihi kwa Mafanikio