“Hamisi: Licha Ya Kutokuwa na Mikono, hategemei mtu”  

Hamisi Lugonda alizaliwa hana mikono lakini anaishi maisha bila kumuegemea mtu yeyote. (Picha kwa hisani ya mtandao)

Japokuwa hana mikono kabisa anaweza kufanya chochote anachotaka kufanya bila kutegemea mtu yeyote yule,anafanya kazi nyingi hata zile ambazo baadhi ya watu wasio na upungufu wa aina yoyote wa viungo hawawezi kufanya. Kwa mfano: kuogelea, kuchunga ng’ombe, kuvua samaki, kulima, kupika,kufyatua matofali, kujenga, kuosha vyombo,kufua,kucheza mpira,kupiga muziki n.k

Umewahi kujiuliza ikitokea huna mikono au miguu utaishije? “Mtu mmoja aliwahi kuniambia kuwa ni vigumu sana kupata jibu mpaka hapo hiyo hali itakapokutokea vinginevyo huwezi kuwa na majibu”. Ni ngumu sana kupata jibu lakini wengine maisha yataishia hapo na kuanza kuishi kwa kutegemea misaada ya wahisani, wengine labda watajiona kabisa kana kwamba hawana thamani kabisa hapa dunianai na kukata tamaa,lakini sitashangaa kama wengine watatumia upungufu huo kuwa fursa na kujitofautisha na watu wengine. 

Nick Vujicic mzaliwa wa Australia ambaye alizaliwa akiwa hana mikono walą miguu aliwahi kusemu hivi: “Ulemavu wa kuogopa siyo mulimavu wa viungo,ogopa saną ulemavu wa mtazamo”

Leo nakuletea kısa cha kijana mmoja mtazania ambaye licha ya kutokuwa na mikono hali ambayo amekuwa nayo tangu alipozaliwa, anaishi maisha ya kujitegemea mwenyewe huku akimiliki vitu vya thamani kuliko hata watu wengi hapa Tanzania na duniani kwa ujumla wasiokuwa na upungufu wa aina yoyote wa viungo.

Namzungumzia Hamisi Lugonda (40) mkazi wilaya ya Nzega mkoani Tabora ambaye ni mlemavu aliyezaliwa akiwa hana mikono yote miwili. Ingawa ilikuwa tukio la kwanza kwa wazazi wake kwani hawakuwahi kuwa na mtoto wa namna hiyo hali hiyo haikuwakatisha tamaa kumlea na kumchukulia mtoto wao kama watoto wengine wenye viongo kamili na hivyo kumpa haki zote za mtoto zilizokuwa ndani ya uwezo wao. 

Sababu za kuzaliwa kwake akiwa mlemavu bila mikono hazikuweza kubainika mara moja kitaalam lakini Hamisi licha ya kuishi kwa kunyanyapaliwa sana na jamii alipoujua ukweli ulimweka huru, na kuamua kujikubali jinsi alivyo na kuishi kama yeye bila kutegemea msaada au kuegemea mahali au mtu yeyote. 

Hamisi anaweza kufanya kazi nyingi hata zile ambazo baadhi ya watu wasio na upungufu wa aina yoyote wa viungo hawawezi kufanya ikiwemo: kuogelea, kuchunga n’gombe, kuvua samaki, kulima, kupika, kufyatua matofali na kujenga nyumba, kuosha vyombo,kufua,kucheza mpira,kuandika kwa miguu na mdomo n.k

Hamisi amekutana na maswaibu mengi katika maisha yake ikiwemo kutengwa na jamii na kuchukuliwa kama mtu asiyekuwa wa kawaida hali ambayo mwanzoni hata yeye ilimfanya ajione kama hana thamani yoyote kutokana na jinsi alivyo. Sasa hivi hadithiya Hamisi imebadilika kwa sababu amekuwa mtu maarufu kutokana na watu wengi kumtembelea kijijini kwake kutaka kujifunza namna anavyoendesha maisha yake bila mikono wala kutegemea mtu yeyote. 

Hamisi anamshukuru sana baba yake ambaye ni marehemu sasa kwamba yeye ndiye aliyemtia hamasa kufanya ajifunze kufanya kazi mwenyewe kwa sababu siku zitakuja ambapo hatakuwa na mtu wa kuweza kumsaidia. “Baba yangu alinisaidia sana na kunifanya nijifunze kufanya kazi nyingi mwenyewe.Alikuwa ananiambia nisipojifunza kujitegemea mwenyewe siku za usoni maisha yangu yangekuwa magumu saną. Kwa hiyo mimi hakuna kitu ambacho nitataka kufanya halafu nishindwe nafanya kila kazi kamą watu wengine wenye viungo kamili” anasema Hamisi aliyefanyiwa mahojiano na mwandishi wa habari wa mtandao wa Milladi Ayo TV aliyemtembelea kijijini hapo kuona anavyoishi. 

Hamisi mwenye mke na watoto wawili aliwahi kukimbiwa na mke wake kutokana na umasikini uliokuwa unamkabili lakini miaka michache baadaye mke wake huyo alirudi baada ya maisha ya Hamisi kuanza kubadilika na kuanza kuishi juu ya mstari mwekundu wa umasikini na hadithi yake ya maisha kubadilika. 

Kutokana na mtindo wa maisha ya Hamisi kuchagua kuishi kinyume na matarajio ya watu wengi leo hii Hamisi ni miongoni mwa watu maarufu wanaotambulika sana duniani kuliko hata watu wanavyoweza kufikiri. Mwezi April mwaka 2021 alitembelewa na waandishi wa habari wa Mtandao wa AfrimaxEnglish hiki ni chombo cha habari mtandao cha nchini uingireza ambao walifika kijijini kwake na kufanya mahojiano naye na hatimaye kurushwa kwenye mtandao wa youtube. Habari ya Hamisi kwenye mtandao huo ni miongoni mwa video zenye watazamaji wengi duniani kwani hadi sasa imetazamwa na watu 13,188,822 na kumfanya kuwa miongoni mwa watu maarufu tayari duniani. Hamisi Lugonda anatembelewa na waandishi wa habari kutoka maeneo mbalimbali duniani na kwa kujulikana huko hali yake ya maisha sasa imebadilika kabisa.

Hamisi ambaye ni baba wa familia anaishi na mke wake na watoto wao wawili wadogo na kwa sasa anamiliki nyumba ya kisasa ambayo alianza kujenga kwa nguvu zake mwenyewe na sehemu kubwa kuungwa mkono na wasamaria wema kutoka ndani na nje ya nchi ambao wameguswa na maisha yake.

Ni kitu gani ambacho umeshindwa kufanya kwa miaka mingi? ni kisingizio gani ambacho umekua ukikitumia kuhalalisha kushindwa kuishi ndoto yako? Je ni hali yako ya kuzaliwa katika familia ambayo unasema masikini? Je una viungo kamili hauko kama Hamisi lakini unaendelea kuhalalisha visingizio vya kwa nini huwezi kuishi ndoto zako? Je! ni hali inayokuzuia kufanza kuishi ndoto zako? Je! kwa namna unavyojiona ukijilinganisha na Hamisi Lugoda wewe ni dhaifu wa viungo kuliko yeye? Hakuna kitu kinachoweza kukuzuia kuishi ndoto yako ili mradi ukikubaliana na hali yako na kujipa zawadi ya kumshuru Mungu. Hujaona sababu bado ya kumshukuru Mungu kwa jinsi alivyokupendelea bila kustahili?

Unapomaliza kusoma ujumbe huu naomba niache swali hapa ambalo nalenga kuibua mjadala mkubwa karibu kama una ujumbe wowote baada ya kusoma ujumbe huu. “Ni kitu gani kinachomtofautisha Hamisi na walemavu wengine ambao hali yao siyo mbaya kamą Hamisi lakini hawawezi kuishi kwa kujitegemea wenyewe? Huwezi kujua thamani ya kitu ikiwa bado unacho mkononi mwako mpaka utakapokipoteza. 

Mtu pekee, kikwazo pekee kinachoweza kukuzuai kufanya unachotaka kufanya au, kwa mtu ambaye unatamani kuwa si kingine isipokuwa ni wewe mwenyewe. Hakuna chochote kinachoweza kukuzuia kuwa mtu unaetaka kuwa. Siyo hali yako, mahali ulipo, au kukosa fursa fulani. Kila kitu kinaanzia kwenye mtazamo wako mwenyewe. 

Kuna wakati tunamwomba Mungu atusaidie tuweze kuvuka na kutimiza ndoto zetu lakini ukweli ni kwamba tunahitaji kujua kuwa ipo sehemu ya wewe kufanya kwanza kabla ya Mungu kuingilia kati kuhusu hali yako. Huwezi kwa mfano kuomba tu halafu ukabweteka lazima maombi yaambatane na kushughulikia kwanza mtazamo wako na kufanya kazi ndipo Mungu sasa ataangilia kati kukunyanyua kupitia kile unachofanya. Kumsubiri Mungu kufanya hata sehemu ya kwako ni kuvunja sheria au kanuni ya kiroho. Watu waliosababisha maisha ya Hamisi kubadilika hawakuja kumtembelea kuona jinsi alivyo mlemavu, bali walivutwa kuja kushangaa matendo ya Hamisi aliyekataa unyonge wa kukaa na kusubiri wasamaria wema ili aishi. Upo mpango mkubwa wa Mungu ndani ya kukuumba jinsi ulivyo.
NI KITU GANI AMBACHO UMEJIFUNZA HAPA?
Ukiwa na watu sahihi unaweza kupita changamoto yoyote kwa urahisi. Hamisi alikuwa na wazazi waliomtia moyo sana katika safari yake ya maisha. Kumbuka hapo juu baba mzazi wa Hamisi alichochea sana mtoto wake kujikubali na kujifunza kushi kwa kujitegemea mwenyewe kwa sababu gani? Alijua kuwa siku moja atamwacha mwanaye na maisha yake asije kuhangaika.
Hamisi mwenyewe alijikubali jinsi alivyo kwa hiyo akachagua kutokumlaumu Mungu wala watu ila kushukuru kwa namna alivyoumbwa na kuangalia anachoweza kufanya hata katika hali yake ya udhaifu na upungufu wa kimwili aliokuwa nao.
Hamisi na baba yake walijua kabisa kuwa aliyekuwa amepungukiwa viungo ni Hamisi wa nje lakini Hamisi wa kiroho au wa ndani yeye hana upunbufu wowote.
Jambo la mwisho Hamisi na wazazi wake walikataa kabisa kusikiliza maneno ya uongo na mitazamo ya watu ambao walimchukulia Hamisi kama bahati mbaya na mtu ambaye hakuwa na thamanini yoyote katika maisha. Badala ya kujielekeza kwenye mambo ambayo hawezi kuyabadilisha, Hamisi alijielekeza kwenye yale ambayo anayataka na Mungu amemjalia sana kuwa mtu maarufu leo mwenye familia yenye furaha na mfano wa kuigwa kwa watu wengine.
Ni muhimu kukumbuka kila siku kwamba changamoto ni sehemu ya maisha yetu nazo hutusaidia kukua na kuwa watu bora zaidi. Changamoto ni kama ngazi ya kutuvusha kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Hakuna anaeweza kukuzuia kuwa mtu unaetaka kuwa isipokuwa wewe mwenyewe.

Naamini kuna kitu cha kukusaidia utakuwa umepata kupitia makala hii fupi. Ukiwa na uhitaji wowote iwe ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako tafadhali usisite kuwasiliana nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini. Unaweza kubonyeza kitufe hapa chini.

Previous
Previous

“Anza Safari: Kuishi Kusudi La Kuwepo Kwako Duniani”