“Anza Safari: Kuishi Kusudi La Kuwepo Kwako Duniani”

Kila binadamu ameumbwa kuwepo hapa duniani kwa kusudi maalum.Kusudi ndicho kitu pekee kinachomtofautisha mtu mmoja na mwingine pia mchango unaoweza kutoa kipindi cha kuwepo kwako duniani. Kutambua kusudi la kuwepo kwako duniani ni hatua muhimu sana katika maisha kwani ndicho kipimo na kigezo cha mafanikio ya maisha ya mtu na humwezesha mtu kuanza kuishi maisha yake mwenyewe. 

Leo nimechagua kukushirikisha mada inayoitwa “Anza Safari: Kuishi Kusudi La Kuwapo Kwako Duniani” na nikushukuru tu kwa muda wako unaotenga kuendelea kufuatilia makala zetu. Nathamini sana mchango wako huo. Haijalishi kama unajua  au hujui kusudi la kuwepo kwako lazima utakuwa na shughuli inayokufanya uishi hapa duniani ambayo inapunguza kila siku muda wako wa kuishi iwe unajua au hata bila kujua. 

Binadamu wote unaowaona unaowajua na wale usiowajua wamegawanyika katika makundi mawili muhimu.Kundi la kwanza ni wale wanaojua kusudi la kuwepo kwao hivyo hawa  wanaishi kusudi lao na kundi la pili ni wale wasiojua kusudi lao la maisha ambapo inawapelekea kuishi maisha ya watu wengine.  Kutegemeana na kundi ambalo mtu yupo kuna watu wanaoishi maisha yao na wengine wanasindikiza wengine kuishi maana hawajui jana,leo wala kesho yao.

KUISHI KUSUDI LAKO

Mtu anayeishi kusudi lake ni yule anayetambua kusudi la kuwepo kwake hapa duniani na kwa kutambua hivyo yeye huishi maisha yake mwenyewe kwa sababu anajua mchango anaopaswa kutoa duniani katika kipindi atakachojaliwa kuishi. Mtu wa namna hii tunasema anaishi maisha yake mwenyewe kwa sababu anajua anakotoka,alipo na kule anakopaswa kuelekea kwa hivyo hawezi kuchukuliwa na upopo au wimbi la mtindo wowote. 

KUISHI KUSUDI LA WATU WENGINE

Kundi lina watu ambao hawajui hata wanakopaswa kufika.Inawezekana wanajua wanakotoka,wanajua walipo lakini hawana picha ya kule wanakoelekea na wakifika wanapaswa kuzaa matunda ya namna gani.

Ni rahisi sana kukasirika pale mtu atakapokuambia haujui unakoelekea ni kama vile amekudharau. Lakini ukweli ni kwamba watu wengi wanaishi katika kundi hili hawajui kusudi la kuwepo kwao kwa hiyo wanaishi kusaidia watu wengine kutimiza kusudi la kuwepo kwao. Kuna watu maelfu kwa maelfu ambao hawana taarifa kwamba wanapaswa kuishi maisha yao kwa hiyo wameendelea kuishi maisha ya watu wengine kwa miaka mingi na pengine kufa wakiwa hawajagusa hata kusudi la kuwepo kwao duniani.  

Mhubiri maarufu hayati Dr Myles Munroe aliwahi kusema kuwa watu wengi wanaogopa sana kufa  ila wanasahau kwamba wanapswa kuogopa kuishi duniani bilakuwa na kusudi kuliko wanavyoogopa kufa kwa kuwa hilo ndilo janga linalokabili watu wengi.  Wapo walioishi duniani wakafa lakini japokuwa wamekufa wangali bado wanaishi kwenye nyoyo za watu kutokana na jinsi walivyotimiza kwa uaminifu kusudi la kuwepo kwao duniani na kutoa mchango mkubwa kwa jamii ambao hauwezi kusahaulika. 

Hawa ni watu kama hayati Nelson Mandela mpigania uhuru na haki za binadamu nchini Afrika kusini na raisi wa kwanza mweusi nchini humo baada ya utawala wa kibaguzi. Japokuwa amekufa hata sasa anaishi katika nafsi za watu wengi duniani kutokana na mambo aliyofanya duniani wakati wa uhai wake.

Ukitaka kujua thamani ya mtu aliyewahi kuishi duniani kama Mandelea hebu jaribu kuweka screen kubwa na kuweka moja ya mkanda wake pengine akihutubia wakati wa uhai wake halafu umweke mtu mmoja maarufa wa nyakati hizi labda mtawala aliye madarakani  atowe hotuba,usishangae kukuta watu wengi wanakimbilia kumsikiliza marehemu na kumwacha mtu anayehutubia live, kwa nini? Kwa sababu maisha yake yaligusa watu wengi duniani wakati wa uhai wao.

Wapo waliofanikiwa kufa wakiwa watupu baada ya kutumia vya kutosha vile vipaji Mungu alivyoweka ndani mwao na wengine wamekufa wakiwa katika namna fulani ya majuto bila kufanikiwa kutimiza kusudi la kuwepo kwao duniani na kuna watu ambao wamefanikiwa maishani mwao kujua kusudi la kuwepo kwao hapa duniani wakiwa wadogo kabisa na hivyo kutoa mchango mkubwa sana tangu wakiwa na umri mdogo karibu uhai wote wa maisha yao na wale ambao wamechelewa kujua kusudi la kuwepo kwao duniani.

Kuna imani iliyojengeka katika jamii kwamba mzee au mtu mzima akishafikia umri fulani basi hawezi tena kufanya chochote.Kwa lugha nyingine ni kwamba mtu katika umri mkubwa hawezi kuishi kusudi la kuwepo kwake duniani kwa kuwa amepitwa na wakati. Huu ni uongo ambao jamii imeaminisha na wengi kujikuta katika nyakati za umri mkubwa wanakata tamaa kwa kuwa tu wamesikiliza watu wa nje wanavyowahukumu kwa uongo. Ndiyo maana watu wengi wanapostaafu wanakubali kuishi ya kana kwamba wanangoja siku ziishe wapite.

UTAWEZAJE KUISHI MAISHA YAKO KATIKA UMRI MKUBWA?

Kutokutambua kusudi la kuwepo kwako ukiwa kijana ni tatizo la watu wengi duniani hivyo hupaswi kuhuzunika kwa kuwa tu umefika mahali pa kustaafu halafu kabla ya kuanza kusudi lako la kuishi. Wewe hutakuwa wa kwanza kupitia hali ya namna hiyo. Haijalishi wewe ni mzee uliyestaafu au unaelekea umri wa kustaafu,nataka kukutia moyo tu kwamba bado unayo nafasi ya kuweza kuanza kuliishi kusudi la kuwepo kwako duniani na kuwashangaza wale wanaokuona kama umekwisha pitwa na muda kuweza kufanya chochote.

Bila kujali maneno ya watu wanayokusemea maneno mabaya kuyaogopa ni yale unayojisemea wewe mwenyewe ndio adui wa mafanikio yako wa kwanza.Kama umetambua kusudi la kuwepo kwako basi hapo safari ya kuanza kuliishi kusudi la kuwepo kwako duniani ndipo itakapoanzia bila kujali una umri gani mafanikio hayana umri. Watu wanapenda kuishi kwa historia badala ya kutengeneza historia. Kama mtu aliwahi kushuhudia katika mazingira fulani watu wa aina yako wakishindwa basi wanachukulia kuwa kibali cha kuhalalisha kwamba watu wote hawawezi. Kuinuka au kuzama kuko mikononi mwako mwenyewe.

Mmiliki wa mgahawa maarufu wa kuuza kuku wa KFC- Colonel Harland Sanders hakuwahi kupata pesa ya maana katika kipindi chote cha kufanya kazi mpaka kustaafu kwake.Alipomaliza muda wake wa kutumika kwa mujibu wa sheria alipewa kiinua mgongo ambacho hakikuzidi dola 180 za kimarekani akajaribu kutaka kujiua baada ya kuamini uongo kwamba kwa kumaliza kazi akiwa na hela kidogo namna hiyo maisha yalikuwa yanafikia ukomo.

Baada ya kupona kujiua alitafakari nini anachoweza kufanya akagundua alikuwa na ujuzi wa kutengeneza kuku hivyo akatumia karibu hela yake yote kuandaa kukua ambapo alipita nyumba baada ya nyumba kujaribu kuuza.Haikuwa kazi rahisi lakini siku alipokuja kukamata soko alistawi sana kupitia bidhaa yake ya kuku.Akiwa na umri wa miaka zaidi ya 60 baada ya kustaafu sasa alikuja kuwa miongoni mwa mabilionea nchini Marekani. Leo migahawa ya KFC imeenea kote duniani.

Hebu inuka funguka kataa uongo wa watu wanaosema umekwishachelewa kuanza kuliishi kusudi lako.Wakati mzuri wa kuanza kuishi kusudi lako hapa duniani ni wakati ule utakapoanza kulitambua kusudi lenyewe na kuamua sasa kuweka vitendo.Utashangaa dunia itakavyoshangilia ujio wa huduma yako ambayo haijawahi kutolewa na mtu yeyote hapa duniani. 

Naamini utakuwa umepata kitu kupitia makala kitu kingine kupitia makala hii fupi. Ukiwa na uhitaji wowote au ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasiliana nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini.Kama kuna namna unafika mahali hujui mahali pa kuanzia ili uweze kupata kutambua kusudi la kuwepo hapa duniani basi tunakukaribisha tuwasiliane tutakusaidia. Bofya mahali palipoandikwa “USHAURI NA MAFUNZO BOFYA HAPA” nasi tutakufikia mapema.


Previous
Previous

“Unataka Kufanikiwa: Chagua Kipaumbele”

Next
Next

“Hamisi: Licha Ya Kutokuwa na Mikono, hategemei mtu”