Tafuta Elimu Kwanza: Kabla Ya Kutamani Kumiliki Pesa Zaidi.

Pandisha uwezo wa kumiliki kabla ya kutafuta pesa zaidi.

Umewahi kukaa chini ukajiuliza kwa nini mtu mmoja ana uwezo wa kumiliki pesa nyingi wala hata kuhangaika na mwingine pesa kidogo tu ikiingia mkononi mwake hatulii mpaka hiyo hela itakapokwisha au ikibaki kiasi fulani basi anatulia? 

Watu wengi pesa nyingi zimepita mikononi mwao lakini hawana hata kitu ambacho wanaweza kuonyesha kamą kumbukumbu kulingana na pesa nyingi iliyopita mikononi mwao. Wakati huo huo kuna mtu anapata pesa kiasi tu lakini anafanya mambo mengi hata wakati mwingine huwezi kulinganisha na kiwango Cha pesa anachomiliki. 

Uwezo wa kukaa na kuhimili kishindo cha pesa siyo jambo la bahati mbaya au kitu kinachokuja tu bila kukiandaa, hapana ni kitu kinaandaliwa hatua kwa hatua. Ukweli ni kwamba watu wote jinsi tulivyo tunapenda kutafuta pesa kwa sababu mbalimbali lakini kila mmoja unaemfahamu na usiemfahamu tuna uwezo binafsi ndani mwetu ambao ndio unaoamua ni kiwango gani cha pesa unapaswa kumiliki kulingana na uwezo wako ili pesa isije kukuletea madhara makubwa. 

Labda niweke hivi uzoefu wangu umenipa kujifunza kwamba hakuna pesa nyingi wala pesa kidogo,isipokuwa ninaweza kusema kuna mtu mwenye maarifa mengi na mwenye maarifa kidogo kuhusu pesa. Hicho ndicho kitu kinachomtofautisha mtu mmoja na mwingine katika eneo hili la kumiliki pesa. Katika safari ya kujitafutia mafanikio ya kifedha, kuna ukweli uliojificha: mafanikio ya kudumu yanajengwa kwanza kwenye akili kabla ya kumiliki pesa nyingi. Ni mienendo, maarifa, na uwezo wa kutumia pesa vinavyotofautisha watu wanaomudu kumiliki kiwango chocote cha pesa na wale wanaopambana kuhimili mzigo wa fedha.

Iko hivi, kuna mtu sasa hivi anafanya dua na kumwomba Mungu usiku na mchana kwa kufunga siku akikamata shilingi milioni 2 tu huo ni muujiza mkubwa kwake Mungu atakuwa amemtendea na kwa kutumia huo muujiza aliopata atakuwa na uwezo wa kufanya mambo makubwa kwa kutumia pesa hiyo. Wakati huo huo kuna mtu mwingine shilingi milioni 2 kwake ni pesa ya kufanyia manunuzi ya mahitaji muhimu ya kawaida nyumbani ambayo anampa mama kwenda sokoni. Maisha ndivyo yalivyo pesa kidogo kwa mtu mmoja kwa mwingine akiishika hiyo ni kama Mungu kamfanyia muujiza. Watu wengi utashangaa hawana tatizo la pesa ila tatizo kubwa ni kukosekana kwa maarifa ya kuishi na kukaa na pesa. Pesa inapaswa kuwa mtumishi wetu itutumikie na walą siyo bwana kwako

Ngoja nikupe ushuhuda huu mfupi ambao umenitokea katika maisha yangu miaka mingi iliyopita. Nikiwa kijana mdogo wa miaka kama 24 hivi nilibahatika kuanzisha kampuni na rafiki yangu mmoja ambaye alikuwa ni mkubwa kwangu kwa miaka kama 12 hivi. Tulianzisha kampuni mjini Arusha ambayo ilikuwa inajishughulisha na utengenezaji, kununua na kuuza sanaa. Ilikuwa ni biashara nzuri sana wakati huo kwa sababu wateja wetu wakubwa walikuwa ni watalii si unajua mikoa ya kaskazini na utalii? 

Tulianza kwa ugumu sana na kama kipindi cha miaka 3 hivi tulihangaika sana kusimama maana kumsingi hatukuwa na mtaji wa kutosha kufanya tulivyokuwa tunatamani. Mungu alitujalia tukaanza kusimama na hatimaye kupata wateja wengi sana. Kipindi chote hicho wakati tunahangaika kutengeneza misingi ya biashara yetu tulifanya mambo kwa maelewano makubwa sana.  Kuna wakati katika maisha afadhali mtu usiwe na pesa nyingi kumbe wala sikuwahi kujua mapema jambo hili. 

Mungu alipotujalia kuanza kupata pesa ndipo sasa tulipoanza kutofautiana misimamo na tabia pia. Yale maelewano tuliyokuwa nayo wakati wa shida sasa yalibadilika kabisa. Mimi nilikuwa sinywi pombe kwa sababu niliikataa tangu nilipokuwa mdogo kutokana na sababu zangu binafsi lakini mwenzangu yeye alikuwa ni mpenzi sana wa kunywa pombe na maswala ya wanawake japokuwa wakati wa dhiki aliishi kwa nidhamu kubwa sana kiasi cha kunifanya nimwamini kwamba anaweza kuwa mshirika sahihi wa biashara. 

Katika shughli zetu tuliweka mgawanyo wa majukumu mimi niliongoza idara ya utawala, fedha na shughuli zote za uzalishaji na mwenzangu yeye alikuwa ni mkurugenzi wa mipango na masoko wa kampuni yetu. Kila mmoja alikuwa kwenye nafasi kulingana na uzoefu aliopitia katika maisha.  Wakati jukumu la mwenzangu lilikuwa ni mipango, kutafuta masoko na kusimamia mauzo, wajibu wangu wa msingi katika kampuni ilikuwa ni kusimamia maswala yote ya uajiri na utawala, fedha na uzalishaji kwa ujumla. 

Mwenzangu alianza kufanya maamuzi ya kutumia pesa peke yake bila kunishirikisha. Tulikuwa na masoko makubwa ya kuuza vinyago na sanaa katika kundi la mahoteli kwenye hifadhi ya Manyara na Ngorongoro zilizoitwa “Serengeti safari lodges”. Matumizi yetu yalianza kuwa makubwa kuliko mapato akienda na mzigo wa shilingi 1,000,000 sokoni kuuza bidhaa ndani ya wiki moja akirudi ametumia hela yote ya mauzo kwa anasa na starehe pengine na deni labda la shilingi laki 5.

Alikuwa akikamata pesa bila kujali ni ya kwake au ya kampuni ataenda bar na kununua pombe kwa kila anaemjua huku akiita wanawake na kuwaambia kama wanataka pesa basi wapandishe nguo aone mapaja na kwa kitendo hicho anamlipa shilingi 5,000. Ndani ya wiki moja ya kufanya fujo pesa inaisha ukikutana naye anatia huruma hana hata pesa ya kula siku moja. Kwa mwendo huo unaweza kujua mwenyewe nini kilichokwenda kutokea kwa biashara yetu. 

Mfano wangu mwenyewe nazungumzia mtu msomi aliyekuwa na cheti kizuri tu cha maswala ya uhasibu na masoko aliyewahi kushika nyadhifa kubwa tu serikalini na katika mashirika kadhaa ya umma. Lakini angalia hakuwa na maarifa ya kutumia pesa kwa tija. Hakujua kabisa namna ya kuishi na pesa kwa hiyo pesa haikuweza kukaa kwake kwa utulivu. Pesa ina tabia na inaendeshwa kwa kufuata kanuni, usipoiwekea kanuni kuiongoza na kufuata yenyewe itakuongoza.

Kwa nini nimeamua kuandika makala hii leo? Kwa kuwa  nimejipa wajibu wa kuongeza thamani kwenye maisha ya binadamu wenzangu naamini msomaji wangu kuna kitu cha kujifunza hapa ambacho kinaweza kukusaidia kufanya maisha yako kuwa bora na kurahisisha safari yako ya kuelekea mafanikio.

Tatizo la huyu jamaa ilikuwa ni uwezo wake wa kubeba pesa ulikuwa mdogo. Ndiyo maana kila pesa ilipozidi uwezo wake basi alijikuta ghafla anapata kichaa cha pesa. Pesa ikipungua na kufikia kile kiwango cha uwezo wake kumiliki kichaa kinaisha hasumbuki tena anatulia.  Huwezi kumimina maji yanayopaswa kujaza pipa kwenye ndoo au kupakia mzigo tani 7 kwenye pickup tani 1 na robo haiwezekani. Kila chombo kitabeba mzigo sawa sawa na uwezo wake wa kubeba. Ndivyo ilivyo hata katika maswala ya maisha na pesa kama uwezo wako unaishia kubeba shilingi milioni 1,000,000 utaumia siku utakayobeba ghafla shilingi milioni 10 kabla ya kupandisha uwezo wako wa kumiliki kwanza. Ndiyo maana ikitokea utahangaika mpaka shilingi milioni 9 iishe ukibakiwa na milioni 1 unatulia maana uwezo wako kukaa na pesa ni milioni 1.

Kama wewe ni kijana au hata mtu mzima bado unasaka mafanikio ushauri wangu ni kwamba kabla ya kuhangaika sana tafuta kwanza elimu ya kupandisha uwezo wako wa kumiliki ndipo uendelee. Inawezekana unajiuliza nitaanzia wapi? Ni rahisi tu anza sasa kujenga nidhamu ya pesa kidogo kidogo inayopita mikononi mwako. Usingoje mpaka upate ile unayoipata pesa nyingi kila kitu kinaanzia kwenye udogo halafu unakua kidogo kidogo. 

Jifunze kidogot kidogot kuwa na pesa na kuishi na pesa kupitia pesa hiyo unayoita ndogo inayopita mikononi mwako. Huwezi kuaminiwa kwa makubwa kabla hujawa na uwezo wa kuishi na pesa kidogo inayopita mikoni mwako. Pandisha kwanza uwezo maana ukiwa mwaminifu kwa madogo hufungua milango ya kuaminiwa kwa makubwa zaidi.

Tatizo siyo kuwa na pesa, tatizo ni kujenga uwezo wako wa kubeba ili ukipata pesa yoyote usikumbwe na ugonjwa unaokumba watu wengi ugonjwa wa kichaa cha pesa. Unaweza kabisa kujifunza kuishi na pesa na kamwe maishani isipate nafasi ya kukusababishia kichaa cha pesa. Naamini kuna kitu cha kukusaidia utakuwa umepata kupitia makala hii fupi. Kama kuna mahali unadhani unahitaji msaaa kujifunza namna bora ya kuweza kuishi na kumiliki pesa bila kukuhangaisha na kuboresha maisha yako katika eneo hilo usisite kuwasiliana nasi kupitia njia hapo chini.  

Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale

WhatsApp: +255784503076

Barua pepe: maishanifursa2017@gmail.com

Previous
Previous

Unao Uwezo Kushinda Vikwazo.

Next
Next

Ninalotaka Silifanyi, Nafanya Nisilotaka!!!