Ninalotaka Silifanyi, Nafanya Nisilotaka!!!

NINALOTAKA SIFANYI ILA HUFANYA LILE NISILOLITAKA

“Umewahi kukutana na mtu halafu akakakuuliza swali hili? “ninalotaka silifanyi,lakini nafanya lile nisilotaka,utanisaidiaje?” hili ni swali ambalo nimekutana nalo mara nyingi nikiulizwa hasa na vijana na leo nimeona niandike hii makala nikiamini kuna namna inaweza kuwa msaada kwa wasomaji wetu wengi”

Ni jambo la kawaida kuwepo mambo ambayo tunatamani kuyafanya na yale ambayo ndani mwetu hatutaki kabisa kuyafanya.Lakini kinyume cha matazamio watu wengi huwa tunajikuta tunafanya yale tusiyoyataka badala ya yale ambayo tunayataka. Hapa ndipo vita kubwa ndani ya nafsi za watu wengi inakoanzia. 

Hebu chukua kalamu na karatasi mbili kaa chini,karatasi ya kwanza uandike yale mambo ambayo huyataki lakini unayafanya na katika karatsi ya pili andika orodha ya yale mambo ambayo moyo wako unatamani sana kuyafanya japokuwa mara nyingi huwa unashindwa kabisa kuyafanya. Hapa ni kale kamsemo “ninalotaka silifanyi nafanya nisilolitaka” 

Ni mambo yale ambayo huwa unayaona kana kwamba hayana uzito sana katika maisha yako lakini yana madhara makubwa sana katika maisha. Kama labda yale unayoyataka unataka kuacha kunywa pombe,unafanya mazoezi na mifano mingine mingi ya namna hiyo. Yale mambo usiyoyataka kama labda kunywa pombe,lakini labda unakunywa badala ya kuacha. Unapenda kufanya mazoezi ya viungo.

Binadamu wote wanayo mambo ambayo hawayataki na yale ambayo wanayata maishani na hayo mambo yote kwa ujumla ndiyo yanayojenga haiba ya mtu. Kwa lugha rahisi tunaweza kuyaita kwa jina moja tu kuwa ni “TABIA”.Yaani zile tabia ambazo tunazitaka lakini hatuzifanyi na zile tabia ambazo hatuzitaki lakini tunazifanya bbila hata kujua.

Binadamu yeyote anapozaliwa anakuwa hana tabia yoyote au tuseme hajui kitu chochote. Huwa ni kama chombo tupu kilichoandaliwa kwa ajili ya kuja kunasa yale maarifa ambayo kitahitaji kwa ajili ya maisha hapa duniani. Mtoto anapokuwa mtupu ana nafasi ya kujifunza hapa duniani akiwa mtoto mdogo na pia atakapokuwa mtu mzima anaweza kujifunza.

Mtoto anapokuwa mdogo tabia na mwenendo atakaoishi katika kipindi chote cha maisha yake hujifunza kwa kuangalia na kutunza kwenye ule umri wa miaka 0-7 ya mwanzo. Hicho ndicho kipindi muhimu ambacho unaweza ama kumtengeneza mtoto ama kumharibu kutegemeana na namna utakavyokuwa umejiandaa kumtengeneza mtu atakayekuwa na tija kubwa kwenye maisha au ambaye atakuwa mwiba kwa walimwengu wenzake. Watoto hujifunza sana kwa watu walio karibu nao wakiwemo wazazi na hata watu wanaowazunguka ambao kwao wote wao hujifunza.

Kwa hiyo unaweza kumwangalia tu mtoto wa mtu jinsi alivyo ukabaini sehemu kubwa ya tabia za wazazi wake zimo ndani yake. KIjana wangu ambaye amemaliza shule ya sekondari mwaka 2019 tulipokuwa tunajifunza somo hili alisema kuwa hakuwahi kuelewa kwa nini mkurugenzi wa shule yao mwanafunzi akikosea kabla ya wazazi alikuwa anawaita wazazi wa mtoto kwanza. Kumbe kwa kufanya hivyo alipata nafasi ya kujifunza wazazi wa mtoto huyo wakoje. Kwa sehemu kubwa wanafunzi wengi hufanana na wazazi wao kwa mambo mengi kwa hiyo kumbe kama tabia za mwanafunzi zilifanana na wazazi wake mkurugenzi wao alitumia njia ya kuwasaidia kwanza wao kabla ya mtoto.

Wanasayansi wanasema 95% ya tabia ambazo tunazo leo tulijifunza wakati tukiwa watoto wadogo. Tafuta mtu yeyote awe rafiki yako,jirani yako,ndugu yako,chunguza tabia zake zile unazopenda na hata ambazo hupendi pale anapozifanya,chanzo chake ni kozi aliyopata bila yeye kujua wakati akiwa mtoto mdogo kutoka kwa wawezeshaji ambao hata wao walifanya hivyo bila kujua. Ukijua jambo hili kamwe huwezi kugombana au kukorofishana na mtu yeyote,kwa nini? Kwa sababu tayari unaujua ukweli kwamba hana kosa lolote maana hiyo tabia usiyopenda aliiokota tangu utoto wake.Alivyo ni matokeo ya maarifa yasiyo sahihi aliyopata akiwa mdogo. Vile vile kwa mtu mwenye tabia chanya chanzo chake ni tangu utoto wake.

Upande mwingine kwa sababu moja au nyingine kama mtoto asipojifunza jambo wakati akiwa mdogo,basi anayo nafasi ndogo ya kujifunza akiwa mtu mzima au baada ya kupita huo umri wa kudaka maarifa kwa urahisi kuanzia miaka 0 hadi miaka 7. Japokuwa kuwa kufanya mabadiliko ukiwa mkubwa kuna ugumu fulani lakini ni jambo linalowezekana. 

Kuna watu wanashindwa kubadilika katika eneo la tabia,ukweli ni kwamba huwezi kubadilisha kitu ambacho hata shina lake ni nini hujui. Ni muhimu kujua chanzo na kiini cha tatizo kabla hujaanza kulishughulikia tatizo lenyewe. Kushughulikia tatizo ambalo chanzo chake hujui inaweza kukuchukua muda mwingi kuliko matarajio. Hivyo ndivyo mtu anavyojifunza kuanzia utoto na hata akiwa mtu mzima. 

Kuna mambo ambayo ulijifunza ukiwa mtoto mdogo mpaka ukamiliza chuo na kuanza kazi ukaja kujifunza tabia ambazo hukuwa nazo tangu utoto wako.Tuseme umekulia katika familia ya wacha Mungu na moja ya tabia ambazo hawakukufundisha ni matumizi ya pombe ya aina yoyote. Hukuwahi kuona wazazi wako wala ndugu zako wanakunywa pombe lakini unapomaliza chuo na kupata kazi unaanza kujitegemea hapo unajifunza sasa ulimwengu mwingine unavyoendeshwa. Marafiki zako wote ni walevi.Kila ukitoka kazini unaambatana nao kwenye maeneo ya pombe. Unaweza kuvumilia kunywa soda mwezi wa kwanza,wa pili lakini mwezi wa tatu unaanza kushawishika kuonja kidogo ili kuwafurahisha rafiki zako maana hawajisikii vizuri wewe ukinywa soda na maji wakati wao wanakunwa pombe. Unaanza kunywa nusu bilauli,kesho unakunywa nusu chupa baada ya wiki 2 unaweza kunywa hata chupa mbili na mwisho ndani ya miezi mitatu unaweza kunywa na kurudi nyumbani ukiwa unachanganya lugha unapoongea. Mchakato ni huo huo hata ukiamua kuwa mzinzi,mwizi,mvutaji n.k

Njia rahisi ya kuvunja au kujifunza tabia mpya ni kufanya mazoezi.Wataalam wanasema ukifanya jambo kwa kurudia ndani ya siku 21 inageuka kuwa tabia na ikiwa tabia unafanya bila hata kusukumwa na mtu yeyote. Ulianza kunywa kidogo kidogo kamwa vile unaonja tu. Ukaanza kurudia,ukarudia,ukarudia mpaka pale ulipofika mahali pa wewe kuwa mtaalam wa kunywa pombe. Ulichokuwa unafanya ni zoezi la kubadilisha tabia kutoka kutokunywa pombe hadi sasa kuwa mnywaji.Tena unaweza kuwa mnywaji wa hovyo kuliko hata wale uliowakuta wakinywa.

Watu wengi wanashindwa kufanya kile wanachotaka badala yake wanafanya kila ambacho hawakitaki! Bila kujua kile wanachopambana nacho wataanza na kuishia njiani. Wanashindana na tabia ambayo imejengwa muda mrefu tangu walipokuwa watoto wadogo sasa haiwezi kuwa rahisi tu lazima kuwepo na mkakati wa kutoka hapo. Wengine huanza na kuishia njiani ni kwa sababu wanahangaika kutibu kitu kingine badala ya kutibu chanzo cha tatizo. 

Naamini utakuwa umepata kitu kingine kupitia makala hii fupi.Kama kuna chochote ulichopata umejifunza basi naomba nisaidie kusambaza kwa wle unaowapenda. Ukiwa na uhitaji wowote au ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasiliana nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini.Aidha kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno au whatsapp au piga simu au email tutapokea na kurudi kwako mapema kadri itakavyowezekana.

Previous
Previous

Tafuta Elimu Kwanza: Kabla Ya Kutamani Kumiliki Pesa Zaidi.

Next
Next

Jifunze Kupitia Makosa.