Hatua 3 Muhimu Kuanza Kufanikiwa Maishani.

Mawazo yako msingi wa maisha yako

“Umewahi kujihisi kama unajitahidi saną lakini maisha hayaendi unavyotaka?, basi makala hii ni kwa ajili yako. Kuna hatua tatu ambazo kila mtu anahitaji kuzizingatia ili kuacha kushindwa na kuanza kujenga mafanikio ya kweli. Hatua hizi ni rahisi, lakini zenye nguvu kubwa sana: Mawazo, Maamuzi, na Matendo”

Watu wengi hutamani kufanikiwa katika maisha wanapoona picha nzuri za watu waliopiga hatua kubwa maishani—wakiwa na biashara au huduma zao, familia zenye furaha, maisha ya utulivu, na wakiwa na heshima na sauti katika jamii. Lakini ni wachache wenye ufahamu kuwa kufanikiwa au kutokufanikiwa siyo tukio la ghafla, bali ni mrejesho wa mchakato uliofanyika ndani ya mtu kwa muda mrefu. Ni matokeo ya kile kilichopandwa ndani ya moyo, akili, na maamuzi ya mtu ya kila siku.

Katika maisha, kila mtu hufanya maamuzi—yawe makubwa au madogo—kila siku. Wengi huyaona kama mambo ya kawaida, lakini ukweli ni kwamba, maamuzi tunayofanya kila siku, kwa kujua au kwa kutokujua, ndiyo yanayojenga hatima yetu ya maisha. Hatima haiji tu kwa bahati au maombi pekee; inajengwa kwa msururu wa mchakato wa ndani unaoanzia kwenye mawazo, kuingia kwenye maamuzi, na kuonekana wazi katika matendo.

Baadhi ya watu walioko katika hali ngumu sasa, inaweza kuwa waliwahi kufanya maamuzi fulani ambayo hayakuwa sahihi. Labda walipuuzia ushauri, walikimbilia njia ya mkato, au waliongozwa na tamaa badala ya hekima. Na matokeo—ambayo wengi huyaita “kutokufanikiwa”—yakawa ni mrejesho wa kile walichoweka ndani yao kwa muda mrefu bila wao kujua.

Kwa hiyo leo, nataka nikushirikishe mambo matatu ya msingi ambayo ukiyazingatia kwa moyo wote, yataanza kubadili mwelekeo wa maisha yako kabisa. Mambo haya siyo mageni masikioni mwako kwani tunaishi nayo kila siku wakati mwingine bila hata kujua kwa namna gani yanaweza kuwa na madhara chanya au hasi kwentu.

1. MAWAZO – Kiwanda cha Hatima Yako

Mungu alitupa zawadi ya kipekee—ubongo. Ndani ya ubongo kuna uwezo mkubwa wa kufikiri, kubuni, kupanga, na kuona mbali. Ndani ya kila binadamu kuna kiwanda cha kuzalisha mawazo, mazuri au mabaya. Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba, watu wengi hawatumii vizuri kiwanda hiki walichopewa na Mungu bure.

Wanasayansi wanasema binadamu wengi hutumia chini ya 10% ya uwezo wao wa ubongo. Hii ina maana kuwa, bado kuna kiwango kikubwa sana cha nguvu ndani yako hujaitumia—na ndio maana maisha yako yanaweza kubadilika kwa kasi kubwa ukianza kutumia uwezo wako ulionao vizuri.

Ukitaka kufanikiwa, anza kufikiri au kuwaza tofauti. Jifunze kufikiri kwa kina, si juu juu. Watu wanaowaza kushinda huona fursa hata pale wengine wanapoona hatari. Mawazo yako ni kama kamba ya mnyama anayepewa nafasi ya kula majani. Mnyama atakula tu ndani ya urefu wa kamba. Vivyo hivyo, hutafika mbali zaidi ya kile unachojiruhusu kufikiri.

Kama kila siku unawaza kushindwa, kuchoka, kuachwa, au kudharauliwa—utajikuta ukiishi maisha hayo hayo bila kubadilika. Lakini ukiwaza kutimiza ndoto zako, kubadili maisha yako na ya wengine, na kusimama imara hata unapopitia katika changamoto—utajenga maisha hayo unayowaza. “Hatima yako iko ndani ya mawazo yako”

2. UAMUZI – Njia Panda ya Maisha

Baada ya kuwaza, hatua inayofuata ni kuamua. Uamuzi ndiyo daraja tunalotumia kuvuka kutoka kuwaza kwenda kwenye uhalisia. Hili ni eneo ambalo linabeba uzito mkubwa sana katika mafanikio ya mtu yeyote.Vitu vyote unavyoona sasa ikiwemo magari, viwanda, majengo marefu,meli, ndege n.k ni matokeo ya mawazo ya watu wakati fulani.

Mungu alitupa utashi na uhuru wa kufanya maamuzi, kwa upekee na heshima hiyo kubwa aliyotupa, hata Yeye mwenyewe haingilii maamuzi yetu moja kwa moja. Lakini jambo la kukumbuka ni kuwa, maamuzi tunayofanya huwa na matokeo—yawe mazuri au mabaya.

Watu wengi huamua mambo ya maana wakiwa kwenye hasira, woga, tamaa na mihemko. Matokeo yake, maisha yao hujaa majuto. Siri ni moja tu: fanya maamuzi yako baada ya kufikiri kwa kina. Usikimbilie kufanya maamuzi kwa kushinikizwa na mazingira au watu.

Maamuzi mazuri yanaletwa na mawazo mazuri. Ukifikiri vizuri, utaamua vizuri. Ukifikiri vibaya, utaingia kwenye maamuzi mabaya. Na maamuzi mabaya ni mbegu ya matatizo mengi ya baadaye.

Kama leo maisha yako hayaendi unavyotamani, ni wakati wa kutathmini: Je, kuna maamuzi niliyowahi kufanya bila kufikiri vizuri? Na kama ndio, basi bado una nafasi ya kufanya maamuzi mapya—mazuri, yenye mwelekeo sahih na kubadilisha maisha yako kabisai. Hauhitaji mwezi, wala mwaka au miaka kubadilika unahitaji kitambo kidogo tu kufumba na kufumbua kubadili unavyowaza na hapo kubadilisha maisha yako.

3. MATENDO – Kipimo Halisi cha Mafanikio

Baada ya kuwa na kufanya maamuzi tayari ni muhimu kukumbuka kuwa hakuna mafanikio bila matendo. Unaweza kuwa na mawazo bora kabisa. Unaweza kufanya maamuzi ya kipekee. Lakini kama hautachukua hatua—kama hautatenda—basi hayo yote yatabaki kuwa ndoto tu.

Matendo ni kiungo kinachofunga mnyororo wa mabadiliko. Ni kama kusafiri kutoka kwenye ndoto hadi kwenye uhalisia. Watu waliopiga hatua kubwa huwa hawaishii kukaa na kuwaza tu —bali huchukua hatua. Wanajaribu. Wanaanguka. Wanasimama tena. Wakatembea hata kama hawakuwa na uhakika wa hatua ya mwisho.

Matendo ndiyo yanayoleta mrejesho halisi katika maisha. Kama unafanya mambo madogo madogo kila siku, kwa nidhamu na malengo thabiti, utapata matokeo makubwa baadaye. Kama unafanya mambo kwa kubahatisha, au hutendi kabisa, basi ni vigumu kuona maendeleo na matokeo yoyote katika maisha yako.

Ujumbe wangu kwako ni huu: Usikae tu ukitazama wengine wakifanikiwa. Usitumie muda mwingi kuwaza tu, au kujilaumu na kulaumu wengine. Simama, chukua hatua, tenda. Fanya jambo hata kama ni dogo leo—kwa sababu matendo madogo ya leo ndiyo msingi wa mafanikio yako makubwa ya kesho.

Mafanikio Ni Matokeo ya Ndani Yako

Kufanikiwa au kutokufanikiwa siyo jambo la nje—ni mrejesho wa kile kilicho ndani yako. Ni matokeo ya namna unavyowaza, maamuzi unayofanya, na matendo unayochukua. Kwa hiyo, kabla hujauliza kwanini maisha yako hayaendi kama unavyotaka, ni muhimu ukaanza kujiuliza:

  • Nimekuwa nikiwaza nini?

  • Nimekuwa nikifanya maamuzi gani?

  • Nimekuwa nikitenda kwa kiwango gani?

Maisha bora yanaanza na mabadiliko ya ndani. Badili mawazo yako, fanya maamuzi sahihi, tenda kwa ujasiri—na utaona matokeo bora zaidi maishani mwako.“Hatima yako haitegemei dunia ilivyo, bali jinsi unavyoamua kuiishi kwa mawazo, maamuzi na matendo yako mwenyewe.”
Naamini utakuwa umepata kitu kupitia makala kitu kingine kupitia makala hii fupi. Ukiwa na uhitaji wowote au ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasili nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini. Aidha kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno, whatsapp kupiga simu au kututumia barua pepe nasi tutarudi kwako mapema iwezekanavyo. 

Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale

WhatsApp: +255784503076-

Email: maishanifursa2017@gmail.com

Previous
Previous

Jinsi Uaminifu Unavyoweza Kuleta Mafanikio ya Kweli Katika Maisha.

Next
Next

Kustaafu Ni Mwanzo Mpya siyo Mwisho