Jinsi Uaminifu Unavyoweza Kuleta Mafanikio ya Kweli Katika Maisha.

Picha kwa hisani ya mtandao

Kuna swali moja muhimu sana ambalo kila mtu anapaswa kuchukua muda kujiuliza: "Je, maisha yangu yanakua?" Kukua ni dalili ya uhai na maendeleo. Watu hukua—kikamilifu au kiroho, kibiashara au kiakili. Mimea hukua. Huduma hukua. Na kila kilicho hai kinapaswa kukua kulingana na muda kilichokuwepo. Ukiona kitu hakikui, kuna tatizo mahali fulani. Na mara nyingi, tatizo hilo lina mizizi yake katika jambo moja: uaminifu.

Uaminifu: Ni Zaidi ya Kuwa Mkweli kwa Wengine

Watu wengi wanapozungumzia uaminifu, hufikiri ni kusema tu ukweli. Lakini uaminifu ni zaidi ya hayo. Ni tabia ya kuwa kweli kwa kile unachoamini, kufanya kile ulichosema utafanya, na kushikilia misingi yako hata kama hakuna mtu anayekuona. Ni kuwa mwaminifu kwa muda wako, kwa pesa zako, kwa ndoto zako, na zaidi ya yote, kwa nafsi yako mwenyewe.

Kukua Bila Uaminifu? Haiwezekani.

Ukitazama kwa makini, utagundua kwamba watu wanaofanikiwa sana si wale walioanza na mtaji mkubwa au elimu kubwa, bali wale waliojifunza kuwa waaminifu kwa kile walichokianza. Wanafuata ratiba zao. Wanatimiza ahadi walizotoa kwa wengine na kwao wenyewe. Hawabadiliki kila mara kulingana na upepo wa mazingira. Wana misimamo thabiti.

Na hii ndiyo sababu biashara nyingi hazifiki miaka mitatu. Ndiyo sababu huduma nyingi nzuri zinafungwa. Ndiyo sababu watu wengi hushindwa kuendelea na mwelekeo waliouanza. Uaminifu umepungua.

Uaminifu Ni Msingi wa Maendeleo

Uaminifu si kitu anachozaliwa nacho mtu. Ni tabia inayojengwa hatua kwa hatua. Inaanza kwa mambo tunayoona madogo madogo:

  • Kuamka kwa wakati uliopanga.

  • Kutoa huduma bora hata kama hakuna anayekupongeza.

  • Kutokutumia pesa ya maendeleo kwa matumizi yasiyopangwa.

  • Kusimama na msimamo wako hata ukiwa peke yako.

Unapokuwa mwaminifu kwa mambo haya, unajiandaa kubeba mambo makubwa zaidi. Biblia inasema, "Aliye mwaminifu katika dogo ataaminika katika kubwa." (Luka 16:10)

Usimtafute Mchawi—Tafuta Uaminifu

Unapojikuta kila jambo linakwama, usianze kulaumu watu, mazingira, au uchumi. Jiulize kwanza: “Je, nimekuwa mwaminifu kwa ndoto yangu? Kwa muda wangu? Kwa kile nilichoahidi kufanya?” Watu wengi hawakui kwa sababu wanajisaliti wao wenyewe kila siku.

Anza Leo Kujenga Uaminifu

Uaminifu ni chaguo. Leo unaweza kuchagua kuwa mwaminifu kwa jambo moja dogo. Kila siku utajenga tabia hiyo. Na kabla hujajua, utaanza kuona mabadiliko makubwa maishani mwako. Utavutia watu waaminifu kama wewe, utaaminika zaidi, na milango mingi itaanza kukufungukia.

Jiulize: "Ninaweza kuwa mwaminifu kwa jambo gani leo?" Anza hapo. Jenga tabia hiyo kwa hatua ndogo kila siku. Utashangaa jinsi maisha yako yatakavyopata mwelekeo mpya. Kumbuka, uaminifu siyo kitu cha watu wakubwa, bali ndicho kinachowafanya watu wa kawaida kabisa kuwa wakubwa.
Uaminifu si jambo la hadithi tu—ni mtindo wa maisha unaojengwa kwa maamuzi madogo ya kila siku. Uaminifu wako kwa muda, kwa watu, kwa kazi, na hata kwa ndoto zako ni mbegu unayopanda kwa ajili ya mavuno ya kesho. Uaminifu hauhitaji jukwaa bali moyo wa kweli.

Jiulize: "Ninaweza kuanza kuwa mwaminifu zaidi wapi leo?" Maendeleo ya kweli huanza pale mtu anapoamua kuwa mwaminifu katika hatua yake ya sasa, hata ikiwa ni ndogo. Mungu anavutiwa na mtu mwaminifu zaidi ya mwenye uwezo mkubwa bila uaminifu.
Kumbuka Uaminifu si kitu cha watu wakubwa, bali ndicho kinachowafanya watu wa kawaida kuwa wakubwa.

Tafadhali acha maoni yako chini au shirikisha na mtu mmoja unayemjua anayetafuta kukua katika maisha yake.
Naamini utakuwa umepata kitu kupitia makala hii fupi. Ukiwa na uhitaji wowote au ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasili nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini. Aidha kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno, whatsapp kupiga simu au kututumia barua pepe nasi tutarudi kwako mapema iwezekanavyo. 

Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale

WhatsApp: +255784503076-

Email: maishanifursa2017@gmail.com

Previous
Previous

Uaminifu kwa Watu Wengine: Msingi wa Mahusiano na Maendeleo.

Next
Next

Hatua 3 Muhimu Kuanza Kufanikiwa Maishani.