Kustaafu Ni Mwanzo Mpya siyo Mwisho
Dr Charles Eugster mwandishi wa kutabu “Age is just number”
Ni mzee aliyeamua kuanza kuishi ndoto yake kwa kuanza mazoezi ya kujenga mwili akiwa na umri wa miaka 87.Ni mwanariadha aliyeshikilia rekodi ya ushindi wa mbio za mita 400 na 600 katika kundi la watu wa umri wake.Alishikilia rekodi za ushindi 4 mbili nchini Uingereza za dunia katika umri wa miaka zaidi ya 90. Ni mwandishi wa kitabu cha "Age is Just Numbers" alichokiandika akiwa na umri wa miaka 95.
Nini kinachokuja haraka kichwani mwako kila unapofikiria kuwa umri wako unasogea na unakuwa karibu zaidi na muda wako wa kustaafu kufanya kazi ya kuajiriwa au kujiajiri? Haijalishi kama unafanya kazi ya kuajiriliwa au umejiajiri mwenyewe lakini ukweli unabaki palepale kuwa unaelekea kuzeeka na kufikia wakati ambao utakuwa huwezi kufanya yale mambo ambayo ulikuwa unaweza kufanya ukiwa kijana.
Mwili unaelekea kuchoka ambapo hutaweza tena kuamka asubuhi na kuingia kazini,hutakuwa tena na kipato chako cha kawaida ulichokuwa umezoea kupata kila mwisho wa mwezi,huna tena gari la ofisi na dereva kama ambavyo mwajiri wako alikuwa amekuweka,huna tena marupurupu na kinga mbalimbali za maisha ulizokuwa nazo, ikiwemo bima ya afya. Lakini kitu unachosahau ni kwamba tofauti na wakati ule ama uliokuwa unaanza maisha au unaanza kazi wakati wa ujana wako,sasa hivi unao uzoefu wa kutosha wa kufanya kitu chochote ambacho utaamua kufanya.
Najua pengine wewe ni miongoni mwa watu ambao wanaamini kuwa kustaafu ni mwisho wa karibu kila kitu ambacho mwanadamu amekuwa akifanya kwa zaidi ya miaka 30 ya ajira yake. Ni mwisho wa kuushughulisha mwili na kazi za kila siku ambazo umefanya tangu ulipokuwa kijana mdogo; wala siwezi kukushangaa hata kidogo maana watu wengi ndivyo wanavyowaza.
Umewahi kuwaza kwa nini mtu mmoja anajiajiri na kuendesha maisha yake yote tangu ujana hadi uzee bila kutetereka katika siku zake za uzee lakini mwingine anaajiriwa huku akijawa na hofu kubwa ya namna atakavyoishi katika maisha yake ya uzee ama baada ya kile kinachoitwa ajira? Tofauti haiko mahali pengine zaidi ya mtazamo! Hapa leo nakuletea simulizi ya mtu ambaye aliishi maisha ya furaha na kuanza kuishi ndoto zake akiwa na umri wa miaka 87.
Wakati unahangaika kujiuliza namna utakavyoishi baada ya kustaafu sasa hivi kuna mtu anafikiria namna atakavyoanza kuishi ndoto zake na kugusa maisha ya watu wengine katika umri mkubbwa ambao wengine wanaona ni kama mwisho wa kila kitu.
Hakuna kilichomzuia kuanza kuishi maisha ya ndoto yake wala hakujali kabisa umri mkubwa kuwa kikwazo kwake kwa sababu aliiona kesho yake kuwa na mambo makubwa kuliko ambavyo aliwahi kuishi katika kipindi chote cha maisha ya ujana wake. Wakati wengine kwa umri wake huwa wanaona mwisho,yeye aliuona mwanzo mpya wa kufanya chochote ambacho angetaka kufanya katika maisha.
Ni jambo la kustaajabisha kidogo wakati unaona kwa umri wako wa miaka 60 kuwa sasa wewe ni mzee ambae pengine huwezi kufanya kitu chochote tena,leo hii kuna mzee wa miaka zaidi ya 80 ndiyo kwanza anaanza kuisha maisha yake mapya na anachukua medali na tuzo kadhaa katika umri huo mkubwa.
Alianza kufanya mazoezi ya kujenga mwili (viungo) akiwa na umri wa miaka 87 na miaka minane baadaye alikuwa tayari ni mtu maarufu duniani aliyejizolea tuzo kadhaa huku mwili wake ukiimarika kama kijana mwenye umri wa miaka 40.Ulikuwa huwezi kutofautisha mwili wake na kijana maana alikuwa amejaa vizuri kutokana na mazoezi ya viungo ambayo alikuwa anafanya kila siku.
Siku zote kauli yake ilikuwa kustaafu siyo mwisho wa maisha ila ni mwanzo wa maisha mapya na kwa kuwa alikuwa na sababu kubwa ya kuamini na kufanya hivyo, alijijengea nidhamu fulani ya maisha, ambayo aliamua kuitii bila kushurutishwa na mtu yoyote na hicho ndicho kilikuwa chanzo cha matokeo chanya ya afya yake kwa kuimarika mwili na akili pia.
Namzungumzia Rain wa Uingereza Dr Charles Eugster mtaalam wa magonjwa ya meno aliyejizolea umaarufu kwa karne hii kwa kuamua hatma ya kuendesha na kuwajibika na afya yake mwenyewe. Mzee huyu ni mfano wa kuigwa na wengi ambaye alifanikiwa kuvunja mfupa uliowashinda wengi na kuukanusha uongo ulioenea kwa miaka mingi kuwa ukiwa na umri mkubwa huwezi kufanya chochote kuimarisha mwili na afya yako.
Nanukuu “Kuzeeka kwa mafanikio kunahitaji kazi, chakula na mazoezi. Uwezo mkubwa wa kiakili na kimwili wa wazee bado haujatumika. Miili sasa inaweza kujengwa upya katika umri wowote na maisha mapya yalianza. Wafalme wa urembo na malkia katika jamii ya umri wa miaka 80 au mwili wa pwani akiwa na umri wa miaka 94 hauwezi kushinikiza. Sote, bila kujali umri wala hali, tunapaswa kuchukua jukumu kubwa kwa afya zetu wenyewe ili kukabiliana na changamoto kubwa zinazoikabili jamii ya binadamu” mwisho wa kunukuu.
Mzee huyu aliayekuwa na kawaida ya kufanya mazoezi kila siku katika enzi za uhai wake, alijizolea umaarufu mkubwa katika kipingi chote cha uhai wake na kubaki kwa mfano wa kuigwa na wengi.
Alishinda zaidi ya tuzo 100 za michezo ya mazoezi ya mwili katika fani mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa mwili na uendeshaji wa mitumbwi. Vilevile, alipata medali nyingi kwenye mashindano ya World Masters Regatta. Hakuna kinachoweza kukuzuia kuanza kuishi zako ili mradi ukiamua kukataa uongo wa dunia kwamba kwa umri mkubwa huwezi kufanya. Je wewe ni mtu mzima ambaye una umri mkuwa ambaye umekuwa ukishindwa kuishi ndoto za maisha yako lakini unasita? Mfano huyu wa Dr Charles Eugster uwe chachu kwako kukuaidia kutoka mahali ulipokuwa umekwama. Hakuna kinachoweza kukuzuia kuishi maisha unayotaka na Dr Charles Eugster ni mtu wa kutiliwa mfano. Alikufa mwaka 2017 akiwa na umri wa miaka 97 huku akiacha jina lake limeandikwa kwa wino usiofutika kazi ambayo alifanya aada ya kustaafu kazi ya kuajiriwa.
Naamini utakuwa umepata kitu kupitia makala makala hii fupi. Ukiwa na uhitaji wowote wa ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasiliana nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini. Aidha kwa email, kutuma ujumbe mfupi wa maneno au whatsapp au piga simu.
Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale
WhatsApp +255784503076
Email: maishanifursa2017@gmail.com