Kama Una Tabia Hii Unasaidia Wengine Kuishi.

Picha Kwa Hisani Ya Mtandao

Kwa nini mtu mmoja anafanikiwa kumiliki muda wake na kuweza kuonyesha matunda ya namna alivyotumia muda wake vizuri na wakati huo huo mwingine anahangaika namna ya kutawala na kutumia muda wake vizuri?

WATU wengi wanajua kwamba muda ni mali ingawa matendo wanayofanya hayaonyeshi kuunga mkono imani hiyo, na imani bila matendo ni sawasawa kabisa na mtu asiyeamini bado kitu chochote.

Muda ndicho kitu pekee cha thamani kubwa ambacho kila mtu anayeishi amepewa kama zawadi bure na Mungu.Kila aliyepewa zawadi hii imeambatana na uhuru wa kuchagua namna anavyotaka kutumia muda wake mwenyewe, bila mtu mwingine kumwingilia kuchagua kwa niaba yake. 

Mtu anaweza kukushauri kutumia muda wako katika eneo fulani,lakini mwisho wa siku ukitekeleza jinsi alivyokushauri utakapokosea hatalaumiwa aliyekushauri kwa sababu ulifanya uamuzi mwenyewe bila kulazimishwa.

Uhuru huo wa kuchagua jinsi mtu anavyotaka kutumia muda wake umewagawa watu katika makundi mawili makubwa;wapo waliochagua kutumia muda wao kutimiza kusudi la kuwepo kwao hapa duniani; na wapo wale waliochagua kuutumia muda wao kusaidia  kutimiza kusudi la watu wengine.

Watu walio katika kundi la pili ndio wale waliokufa au watakaokufa bila hata kugusa kusudi binafsi la kuwepo kwao hapa duniani,kwa sababu muda wao mwingi wanautumia kusaidia kutimiza kusudi la watu wengine.Hebu fikiri muda una mwisho na siku moja isiyo na jina utakuwa mbele ya hakimu ukitakiwa kutoa hesabu ya namna ulivyotumia muda wako ulipokuwepo hapa duniani! Utakuwa miongoni mwa watu waliopoteza muda au waliotumia muda wao vizuri na kustahili tuzo?  

Uhuru umepelekea wengine kuchagua vizuri matumizi ya muda wao na wengine kwa kujua na hata baadhi bila kujua kujikuta wamechagua vibaya namna ya kutumia muda wao; na bahati mbaya sana moja ya sifa muhimu ya muda ni kwamba muda una muda wa kuwepo na muda wa kwisha. Muda siyo kitu cha kukaa milele upo wakati utakuwa na muda na upo wakati utatamani kuwa na muda lakini hutakuwa nao.

Muda ni eneo ambalo nimehangaika sana nalo katika kipindi kirefu cha maisha yangu kabla sijagundua na kuanza kuchukua hatua kuwa bora katika eneo hili. Kwa kuwa nimejipa kazi kipindi cha maisha yangu kilichobaki nifanye kazi ambayo itagusa maisha ya watu wengine, basi natamani kugusa maisha ya watu wengi wanaohangaka katika eneo la muda.

Nimeeleza katika aya iliyotangulia ili ujue kwamba mtu anayewasiliana na wewe kupitia makala hii, anao uzoefu katika swala la muda na usisahau uzoefu ni mchanganyiko wa kushindwa na kushinda katika eneo fulani.

 Kuna msemo ambao sikumbuki asili yake unaosema “kujua tatizo ni chanzo cha kutatua tatizo”, hivyo nataka tutafakari kidogo shughuli zinazokula muda wetu bila kujua; kama kwa kutumia muda wetu mwingi katika shughuli hizo kuna mtu tunamsaidia kutimiza kusudi la kuwepo kwake duniani.

1.Mtandao wa intaneti

Kukua kwa teknolojia kumesababisha mageuzi makubwa sana katika swala zima la mawasiliano ambapo sasa dunia ni kama kijiji. Ingawa Intaneti ni zana muhimu katika maisha ya kisasa lakini intaneti ni kitu ambacho kinatafuna muda wa watu wenye hela na ambao hawana hela. Watu wengi wanaperuzi mtandao mmoja baada ya mwingine kuangalia vitu ambavyo wasipoangalia hawatakutwa na madhara ya aina yoyote.

Makundi mawili ya watu tuliotangulia kuwataja hapo juu wako huku kwenye mtandao kwa makusudi maalum. Kundi la kwanza lile la watu wanaojua kinachoendelea hivyo wanatamani kutumia fursa hii kufanya kitu kutimiza kusudi la kuwepo kwao na wale ambao wana muda mwingi kusaidia wenye malengo kutimiza kusudi la wenzao kuwepo.

Kama una anuani ya barua pepe basi utakuta kuna barua pepe nyingi zinakuja katika sanduku lako hata za watu usiowajua. Wengine wakitangaza fursa na biashara mbalimbali. Nataka nikutahadharishe kama unachukua muda mwingi kusoma email za watu ambao huwajui,wewe ni miongoni mwa watu wale wanaowasaidia wengine kutimiza lengo la watu wengine kuwepo duniani.

2.Mitandao ya kijamii:

Mitandao ya kijamii kama FaceBook, twiter,Instergram,whatsap,youtube n.k inakula muda wa vijana wengi wanatumia muda mwingi kwenye mitandao hii ya kijamii na hakuna hata pesa kidogo wanayopata kwa kushinda kwao kwenye mitandao ya kijamii.Nataka kutoa mifano michache tu hapa ili nieleweke vizuri.

3.FaceBook: Kama wewe ni shabiki na mtumiaji mkubwa unayeshinda kwenye FaceBook inayomilikiwa na bilionea mtoto Mark Zuckerberg jambo usilolijua kila sekunde inayokwenda kwa Mungu unamsaidia kijana huyu kutimiza kusudi la kuwepo kwake duniani na hivyo anatengeneza mamilioni ya dola kila saa inayopita na wewe ni sababu moja wapo.

Kuna watumiaji wenzako wa FB zaidi ya bilioni 1.9 duniani na wengi ni watazamaji hakuna chochote wanachopata, wakati huo bilionea kijana huyu mmmiliki wa FB akimiliki utajiri wa dola Zaidi ya bilioni 56 za kimarekani.

4.Whatsapp: Mtandao wa whatsap una watumiaji Zaidi ya bilioni 1.2 duniani, na lengo la wamiliki wake ni kutoa huduma halafu watengeneze pesa nyingi kadri itakavyowezekana. Kama wewe ni mtumiaji maarufu wa whatsap uwe na uhakika unasiadia kusudi la mtu kuwepo litimie. 

5.Instagram: Kama wewe ni mtumiaji maarufu wa mtandao huu wa instagramu uwe na uhakika kuwa wewe ni miongoni mwa watumiaji wenzako milioni 700 duniani na jamaa wanachotaka kutoka kwako ni kuwasaidia kutoa huduma na hasa kutengeneza pesa kubwa na lengo hilo linatimizwa na watu wengi kuwafuatilia na kutumia mitandao hiyo ukiwemo wewe.

6.Ushabiki wa michezo

Ushabiki wa michezo hasa mpira wa miguu umegeuka kuwa mlaji mkubwa wa muda wa mashabiki hasa vijana ambao ndio wenye nguvu kwa ajili ya uzalishaji na kukuza uchumi wao binafsi na taifa kwa ujumla.Kuna watu kuanzia asubuhi mpaka usiku kichwani mwao wanafikiri sana juu ya mpira bila hata kujali kama wanaingiza kipato chochote kwa ajili ya kuboresha maisha yao.

Ukweli ni kwamba wakati unashabikia mchezaji fulani wenzio wanaingiza fedha kila dakika inayopita.Wakati unabaki kuulea umaskini matajiri wanaomiliki hizo timu wanaendelea kutajirika.Hebu fikiri vizuri namna unavyotumia muda wako kwenye ushabiki wa mipira.Je utaendelea kuishi kwa kusaidia kusudi la mtu mwingine?

Hiyo ni mifano michache ya namna watu wanavyotumia muda wao mwingi kwenye mambo ambayo hayawasadii wao binafsi kuishi ndoto zao,Zaidi ya kusaidia makusudi ya uwepo wa watu wengine hapa duniani.

Usininukuu kwamba ninapinga matumizi ya mitandao ya kijamii hapana natamani tujue namna bora ya kutumia mitandao hii ya kijamii kwa faida badala ya kusaidia watu wengine kuishi ili itusaidie kukuza kusudi la uwepo wetu duniani.

Kama ambavyo una uhuru wa kuchagua namna gani utumie muda wako nataka nikuachie kazi ya kujihukumu uko upande gani kati ya hayo makundi mawili na mwisho majibu ya hukumu yako yakupandishe hasira na kukufanya ujipange upya hujachelewa namna ya kutumia muda wako kwa tija. 

Kama kuna kitu utakuwa umekipata kupitia makala hii fupi ni maombi yangu uanze kupanga namna unavyotumia muda wako kwa uaminifu na uanze kuishi kwa kutimiza kusudi na ndoto zako.

Naamini kuna kitu utakuwa umekumbushwa kupitia makala hii fupi.Kama kwa namna moja au nyingine ungependa kupata ushauri au wa namna ya kuboresha katika eneo lolote la maisha,au kuingia ndani Zaidi ya makala hii,basi usisite kuwasiliana nasi kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno,whatsapp kwa kutumia no ya simu hapo chini.

Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale

+255784503076                                                      
Email:
maishanifursa2017@gmail.com 

Previous
Previous

Kustaafu Ni Mwanzo Mpya siyo Mwisho

Next
Next

Namna Ya Kushinda Tabia Ya Kuahirisha Mambo