Namna Ya Kushinda Tabia Ya Kuahirisha Mambo
Picha kwa hisani ya mtandao
Azimio la kujenga makazi ya kudumu ili kuepuka maumivu yanayosababishwa na hali ya majira kubadilika lilipitishwa tangu enzi za mababu na mababu, lakini limeahirishwa mpaka leo. Siyo babu wala baba zake waliofaulu kutimiza azma ya kujenga makazi ya kudumu.
Jitihada za kujikinga na kukinga watoto wake dhidi ya mvua kali iliyokuwa inanyesha wakati mwingine ziligonga mwamba na kujikuta kila mmoja katika familia ya manyani akihangaika kujitafutia namna ya kujizuia na mvua kali iliyokuwa inanyesha.
Mabadiliko ya hali ya hewa yalimpa kufikiri sana. Kitu gani angeweza kufanya ili kuepuka madhara yanayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa. Kipindi cha kiangazi na jua kali hakuhangaika sana kama alivyohangaika kipindi cha mvua kali.
Ukiwaangalia nyani wana umbo linalofanana sana na binadamu, wana mikono, wanaweza kutembea kwa kusimama kama binaamu, wanapanda miti kwa urahisi kuliko wanyama wengi, ila tu hawana ufahamu kama aliojaliwa binadamu.
Kila mvua iliponyesha nyani kwa uchungu walikumbushana umuhimu wa kujenga nyumba kwa ajili ya makazi ya kudumu hasa wakati ule walipokuwa wamekaribia kutokuwa na namna yoyote ya kujisaidia, mvua ilipopita basi waliahirisha mpango wa kujenga.
Hapo ndipo ulipoanzia ule msemo kesho ya manyani, kwani licha ya kujua kile wanachohitaji na uchungu na hasara wanayoipata wakati wa mvua kali inaponyesha, Nyani wameendelea kuahirisha mpango wa ujenzi wa makazi ya kudumu, azimio la tangu enzi za mababu na mababu na mpaka leo wanahangaika.
Watu wengi tunafanya mambo yanayofanana na mfano huu wa manyani. Ipo mipango tumepanga sasa miaka inapita hatujafaulu kuweza kutekeleza mipango hiyo, kila siku nitafanya hivi kesho, nitafanya hivi, nitafanya hivi na matokeo yake tunajikuta tunashindwa kufikia malengo tuliyojiwekea wenyewe.
Tabia ya kuahirisha mambo yanayowezekana kufanywa leo, kwa ahadi ya kufanya siku nyingine, ni ugonjwa unaowasibu watu wengi na imechangia sana kufisha ndoto nyingi na kubaki kuwa mambo ya kufikirika.
Hakuna wakati mzuri au mbaya wa kufanya jambo unalojisikia kufanya ili mradi ndani mwako kuna amri inayokusukuma kufanya jambo hilo kwa hiara yako mwenyewe bila kusukumwa na mtu. Kila wakati ni sahihi kwa mtu sahihi. Ukipoteza fedha unaweza kuhangaika kutafuta ukazipata ten ahata Zaidi ya zile ulizopoteza.lakini muda pekee ukishapita hakuna namna unaweza kulipia muda uliopotea mpaka utakapokufa.
Tumejiwekea mazoea ya kuona kama muda tulio nao ni mwingi sana na kusahau kuwa muda una ukomo pia.Ukweli ni kwamba watu wote waliofanikiwa ni mameneja wazuri wa muda wao na huwa waangalifu sana kuchagua mambo ambayo yatatumia muda wao kwani muda ni mali kwao.
1. Fanya mabadiliko kwenye akili kwanza
Ukitaka kubadilika katika eneo lolote unapaswa kubadilika kwanza katika mtazamo wako.Watu wengi wamehangaika sana kwa kujaribu kubadilika bila kubadilisha mtazamo,matokeo yake wamejikuta wanatumia muda mwingi sana kufikia azma yao.Huwezi kubadili tabia bila kubadili mtazamo kwanza.
2. Simamia muda wako vizuri badala ya kusimamiwa na muda.
Hakikisha unapanga matumizi ya muda wako kabla hujaanza kuutumia kila siku asubuhi.Kama unavyopanga namna ya kutumia kipato chako ndivyo unavyopaswa kupanga muda wako.Kila saa inayopita ipangie matumizi.Kwa nini? Kwa sababu ukishapoteza muda kuurudisha ni jambo karibu sawa na haiwezekani.
Bila kuweka utaratibu wa namna utakavyotumia muda wako,basi uwe na uhakikika mtu mwingine ambaye kutokana na wingi wa shughuli alizo nazo,amekwisha panga jinsi ya kukutumia muda wako kutekeleza malengo yake.
3. Tekeleza kadri ulivyopanga.
Jitahidi kuhakikisha unatekeleza shughuli zote ulizoweka kwenye mpango wako wa matumizi ya muda bila kuvuruga.Ni muhimu sana kufanya hivi kwani usipofanya hivyo,kuna watu wanatafuta watu wenye muda ambao hauna kazi wakutumie.
4. Fanya tathmini na marekebisho kila inapobidi.
Kamwe usiogope kukosea kosea kadri utakavyoweza ili mradi tu uwe umeshughulikia mtazamo wako vizuri kuweza kuona kwamba makosa hayaji kwa ajili ya kukwamisha ila kukuimarisha na kwani kila unapokosea kuna kitu kipya utakuwa nimepata maarifa muhimu kukuwezesha kufanya vizuri zaidi kesho.
Hakikisha unajiwekea utaratibu wa kufanya tathmini kila siku kabla ya kulala,kila juma na kila mwezi kuona wapi umefanya vizuri na wapi kuna mapungufu ili uweze kuboresha.Fanya hivyo kwa kurudia mara kwa mara mwisho utajikuta inageuka kuwa tabia,na ikiwa hivyo basi huwezi kuona maumivu tena kufanya.
5. Sherekea ushindi
Wataalam wa saikolojia wanasema kama utafanikiwa kufanya kitu kipya mfululizo kwa wiki tatu basi inabadilika kuwa tabia na kama nitabia unaanza kuishi tabia hiyo haiwi tena mzigo kufanya. Endelea kufanya hivyo na sherehekea ushindi.
6. Tafuta Kocha.
Kuna ambao kwa sababu ya mazingira au vinginevyo kutekeleza zoezi hilo inaweza kuwa changamoto,basi ukifika hatua hiyo unahitaji mtu wa kukuelekeza na kukusaidia kuweza kutimiza azma yako ya kuwa meneja wa muda wako.Hapa inabidi umtafute kocha. Kocha ni mtu ambaye wakati mwingine ameishi hali inayokusibu lakini ameshinda na kufaulu kupata namna au teknolojia ya kusaidia mtu mwingine kuvuka mahali alipokwama na kufupisha safari.
Kumbuka kama mpira una kocha hata maisha yanapaswa kuwa na kocha.Jilinganishe na mtu ambaye ungependa ufanane naye katika maisha yako.Hakikisha unaamua kufanya kila utakaloweza kuondoka na ugonjwa wa kuahirisha mambo.
Nataka tu nikukumbushe kwamba mambo yote haya tunayofanya ili kuleta mabadiliko katika maisha yetu kubadilika ni mara moja. Ukitaka kutawala muda wako basi mabadiliko yanaanza pale ulipoweka azma kufanya hivyo. Kinachofuatia ni mkakati kufikia ndoto yako ya mabadiliko. Kumbuka ile tu kuwa katika hali ya uzima na afya maisha ni fursa Mungu aliyotupa na hatuna kisingizio chochote kushindwa kufanya chochote ambacho ungependa kufanya.
Naamini utakuwa umepata kitu kupitia makala makala hii fupi. Ukiwa na uhitaji wowote wa ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasiliana nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini. Aidha kwa email, kutuma ujumbe mfupi wa maneno au whatsapp au piga simu.
Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale
WhatsApp +255784503076
Email: maishanifursa2017@gmail.com