Kazi Ni Nyingi, Ajira Chache!!
Picha kwa hisani ya mtandao
Ingawa watu wengi wanajua kuwa ulimi huumba na mara nyingi kinywa hukiri kile kinachoujaza moyo,hawaachi kukiri na kujitamkia misemo ambayo imezoeleka katika maisha yao na matokeo yake wanaanza kuiishi. Miongoni mwa misemo hiyo ni pale unaposikia watu wanakiri kuwa hakuna kazi siku hizi na kwa kuwa ndivyo wanavyoamini basi,hivyo ndivyo inavyokuwa kwao na nafasi za kazi zinakuwa adimu kweli kweli.
Karibu tena katika makala zetu za kujenga katika mtandao wa www.maishanifursa.com .Kwanza nikushukuru sana kwa kuendelea kutuamini na kufuatilia kazi zetu. Kazi hii ina maana tu kwa sababu wewe upo. Kama ni mara yako ya kwanza kutembelea mtandao wetu,nikukaribishe kwa mikono miwili na kuahidi kuwa hutakaa ujute kuufahamu mtandao huu.
Nilibahatika kukukuta mjadala wa namna hii ukiendelea katika kituo kimoja na mabasi hapa nchini ambapo watu walikusanyika wakalianzisha.Upande mmoja ambao ulikuwa na wafuasi wengi ulikuwa unakubaliana kuwa kwa swala la kazi hakuna kazi siku hizi ikilinganishwa na zamani.
Upande mwingine ambao ulikuwa na watu wachache sana na hata walikuwa hawasikilizwi sana kutokana na uchache wao kulikuwa ulikuwa unakataa kuwa nafasi za kazi zipo za kutosha.
Huwa napenda sana kunyamaza kabla ya kuingilia kwenye mada yoyote ili nipate nafasi ya kujifunza na kuona jinsi watu wanavyowaza. Mjadala ulikuwa ni mrefu na hata mwisho muafaka haukuweza kupatikana kila mmoja alibaki kuamini anavyoamini tu.
Nilijaribu kutaka kuingilia kati kuwasaidia watu hao lakini bahati mbaya hekima ilikataa na hasa nikizingatia kwamba hakuna aliyenikaribisha kuingilia mjadala ule na hakuna aliyenijua.Ingawa nilikosa nafasi lakini kimoyomoyo nilikuwa nalo jibu.
Hiki ndicho kilichonisukuma kuandika makala hii fupi leo ili kutoa kile ninachoamini ni jibu la mjadala huo wa “hakuna kazi”. Hujasikia watu wengi wakilalamika kuwa hakuna kazi na pengine nawe kujaribiwa kuanza kuimba wimbo huo ambao kimsingi haupaswi kukuhusu sana?
Ninachoweza kusema ni kwamba wote wako sawa wanaosema hakuna kazi na wale wanaosema kazi zipo.Hapa hutanielewa mpaka utakaponivumilia kuendelea kusoma mistari michache inayofuata.
Kwa nini nasema wote wako sawa inategemea sana mtazamo wa kila mtu.Yule anayesema kazi hakuna na kweli hakuna kazi itakayojitolea kumfuata kwa sababu tayari ndani mwake amekwisha fanya azimio kuwa hakuna kazi.Na yule anayesema kazi zipo amekwisha fanya azimio kuona fursa za kazi kila anakokwenda.
Ninavyojua mimi kazi ni shughuli yoyote halali ya kukuingizia kipato halali ambayo utaifanya kwa kuipenda.Tafsiri ya kazi haiwezi kuwa ile uliyosomea tu.Wapo watu wengi hapa Tanzania na hata duniani wamesomea kazi nyingine na wanafanya kazi tofauti na ile waliyosomea na maisha yanaenda.
Wanaohangaika kutafuta kazi ni wale waliofunga milango ya kuruhusu fursa zingine kuja upande wao na kujikuta hakuna fursa itakayokuja upande wao kwa sababu wamefunga milango.
Wanaoona fursa za kazi kila wanakokwenda ni wale ambao wamefungua milango ya kupokea na macho yao yanaona uwezekano wa kazi na fursa kila wanakokwenda.
Nini cha kufanya?
Kama wewe ni miongoni mwa watu wanaoamini hakuna kazi siku hizi ningependa kukushauri ubadili mtazamo. Usikae na kusubiri tu mlango wa kazi uliyosomea ufunguke,anzia mahali fulani hata kama siyo ile uliyosomea utaona fursa za kazi zinaanza kukimbilia upande wako.
Wote wako sawa wanaosema hakuna kazi wako sawa kwa matazamo wao na wanaosema kazi zipo wako sawa inategemea sana mtazamo wa kila mmoja.Wakati unalalamika hakuna kazi,kuna watu sasa hivi wanachagua fursa gani wachukue na fursa gani waache kwa sababu fursa za kazi ni nyingi kuliko wanavyohitaji.
Kumbuka ile tu kuwa katika hali ya uzima na afya maisha ni fursa Mungu aliyotupa na hatuna kisingizio chochote kushindwa kufanya chochote ambacho ungependa kufanya,ili mradi uko hai na Mungu ameweka namna ya ubunifu ndani mwako.
Naamini utakuwa umepata kitu kupitia makala hii fupi. Kama utakuwa na uhitaji wowote au ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasiliana nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini.Aidha kwa email,kutuma ujumbe mfupi wa maneno au whatsapp au piga simu.
July 17,2017
Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale
WhatsApp: +255784503076