Kwa Nini Wengi Hushindwa Kuishi Ndoto Zao!

Picha kwa hisani ya mtandao

Kuna tofauti kubwa kati ya mtu anayejua anachotaka kufanya ambaye huthubutu kufanya bila woga na yule ambaye yeye licha ya kujua anapashwa kufanya nini lakini anakosa ujasiri kufanya kwa kuongozwa na hali ya hofu na kusitasita.

Watu wengi wamegawanyika katika makundi mawili makubwa yaani kundi la watu wanaothubutu bila kuweka vikwazo kabla ya kufanya na wale wanaosita kufanya kitu chochote kwa kuhofia kushindwa kabla ya kufanya.

Karibu tena msomaji katika mtandao wetu wa maishanifursa. Leo tutajikita katika mada ambayo nimeipa kichwa “Kwa Nini Wengi Hushindwa Kuishi Ndoto Zao?” Nakushukuru sana kwa kuendelea kufuatilia kazi zetu uwepo wako ni muhimu sana kwa kazi yetu kwani bila wewe kazi haipo. 

Uzoefu unathibitisha kuwa watu wengi waliowahi kuishi na wanaoishi wanaoongoza katika mafanikio,wanaongoza pia kwa kushindwa lakini cha muhimu ni yale masomo muhimu wanayoyapata katika kushindwa kwao ambayo ndio yanayojenga safari yao kuwa ya mafanikio na kuwatofautisha na watu wengine.

Hebu tuangalie sababu tatu kubwa kwa nini watu wengi wanasita kufanya mambo ambayo wanajua kabisa wakifanya yangeweza kubadilisha kabisa maisha yao na kukamilisha safari yao ya mafanikio?  

1. Kuogopa Kushindwa (Feir of failure)

Uoga wa kushindwa ni hali ambayo imepelekea watu wengi kushindwa kufanya kitu chochote kwa kuhofia kushindwa.Jamii imeweka viwango vya juu vya mtazamo ambapo watu mara nyingi umewawekea mipaka na kushindwa kufanya mambo mengi.

Watu wengi hawapendi kujihusisha na kitu chochote ambacho wanahisi kitakwenda kuishia kwenye upungufu ili kuepuka hukumu ambayo imekwishatolewa na mfumo wa jamii juu ya watu wanaoitwa wameshindwa. 

Kwa hiyo njia moja ya kuepuka kujiweka katika hukumu ya jamii ni kukwepa kujaribu kufanya kitu chochote wakiamini kwamba kwa kufanya hivyo wameepuka kushindwa kwa hiyo kuepuka fedheha.  

Maumivu na matokeo ya kusita kufanya yanaweza kuwa mabaya zaidi ya fedheha ya ambayo mtu anaweza kupata baada ya kushindwa kufanya kwa kuogopa tu kushindwa au kuhukumiwa vibaya na jamii.   

2. Kukosa Hamasa (Low Enegy)

Wataalam wa maswala ya kiafya wanasema watu wasio na mtindo mzuri wa maisha huwa na hamasa ndogo  (low energy). Hawajisikii kufanya kitu chochote zaidi na hali hiyo huwaongoza kuazimia kuahirisha mambo. Kama huwezi kupata usingizi wa kutosha au kula chakula ambacho si sahihi,unaweza kujihisi uvivu na uchovu. Mtindo wa maisha wa mtu kinaweza kuwa kichoceo cha mtu kuhamasika kufanya vitu  

Mojawapo ya tabia muhimu ya kawaida ya watu waliofanikiwa ni kuamka mapema kufanya mazoezi  mara kwa mara ambayo husaidia sana kuamsha ari ya kufanya mambo bila kujali kama ku naweza kuwepo kushindwa mbele ya safari. 

Hakuna mtu aliyefanikiwa kwa kuhakikisha anafanya kila kitu kwa ukamilifu ila mafanikio hufikiwa kwa kuweka juhudi na kurekebisha makosa njiani,huku mtu huyo akiwa na uhakika wa kule anakotaka kufika. Njia huweza kubadilika kisichobadilika ni kusudi.

Kwa mfano unaweza kuwa uko Arusha na unataka kusafiri hadi Dar-Es-Salaam mahali fulani.Unaweza kujaribu njia moja na kabla hujafika hata nusu ya safari yako njia hiyo ikawa na changamoto kiasi kwamba haiwezi kukusaidia kufikia lengo lako la kufika DSM,unachobadilisha ni njia ya kufika huko lakini nia yako ya kufika Dar itabaki kuwa ni ile ile.

3. Kutokuwa Na Maono

Kama hujui unakopswa kuelekea na sababu ya kufanya unachofanya,unaweza kuhisi kana kwamba wewe ni kama gurudumu linalojizunguka lenyewe. Kutokuwa na dira ya wazi ya lengo au picha kubwa ni moja ya sababu ya kawaida ya kuhairisha mambo.

Mara nyingi huwa tunajikuta tunasita kufanya na kuweka pembeni mambo muhimu kwa sababu tu hatujui mahali pa kuanzia. Pengine unafanya kazi fulani ambayo unaona ni ngumu na ina usumbufu mkubwa kuifanya ni rahisi kuweka pembeni na kuanza kufanya kazi nyingine. 

Bila kuwa na maono ya kukuongoza kupata matokeo sahihi,unaweza kuishia kujielekeza kwenye matukio ya muda huo yanayojitokeza kama kuangalia ujumbe mfupi wa simu,kuangalia mtandao badala ya kufanya yale unayopaswa kufanya ili kufikia lengo lako.Kuwa na maono thabiti kutakuwezesha kuchukua matendo sahihi.

Sasa Jitoe Katika Gereza La Kusita Anza Kufanya

Kama ujumbe katika makala hii unafanana na ukweli fulani katika maisha yako basi uko mahali sahihi sasa kuanza kutoka kwenye kifungo hicho cha hiari cha kusita na kujiweka katika mazingira kuanza kufanya kile ambacho umekuwa ukisita kufanya kwa muda mrefu.

Unataka kumiliki nyumba yako lakini kwa muda mrefu umekuwa ukisita kwa kigezo kibovu ulichoweka kwamba mpaka upate pesa ya kutosha kujenga,nakwambia anza kufanya hatua kwa hatua kutumia fedha yako unayoipata kidogo kidogo. 

Unajua kama utachukua hatua ya kujiendeleza kimasomo itakusaidia sana kutimiza baadhi ya malengo yako katika maisha lakini kila unapotaka kuanza umekuwa ukisita na kuahirisha kwa kuogopa hatari unazoziona mble yako,nakwambia fumba macho anza kusoma utaona hatari zote unazoishi kwa kudhani zinaanza kukukimbia moja baada ya nyingine. 

Kuna wito mkubwa wa kufanya biashara fulani ndani mwako na hakika uthibitisho ndani mwako unakuambia aina ya ukubwa wa mafanikio utakayofikia mara tu utakapoanza kufanya biashara hiyo ya wito wako,lakini umesita kwa kusikiliza uongo kwamba huwezi mpaka utakapokuwa na mtaji wa kutosha,nakwambia toka gerezani fungua minyororo iliyokuzunguka unachelewa. 

Hakuna mtaji mkubwa wala mdogo fedha yoyote inatosha kuifanya kuwa mbegu na kwa kuwa mbegu ina kanuni ya kuzaa ndani yake basi anzia pele ulipojaliwa kuweza badala ya kusubiri eti uwe na mtaji wa kautosha fanya. Kuna mtazamo mdogo na mtazamo mkubwa siyo mtaji mkubwa wala mdogo.

Naamini utakuwa umepata kitu kingine kupitia makala hii fupi. Ukiwa na uhitaji wowote au ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasiliana nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini.Aidha kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno au whatsapp au piga simu au email tutapokea na kurudi kwako mapema kadri itakavyowezekana.

Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale

WhatsApp +255784503076 

Email:maishanifursa2017@gmail.com

Previous
Previous

Maisha Ni Mradi Wako Mwenyewe!

Next
Next

Kazi Ni Nyingi, Ajira Chache!!