Kitu Hiki Kila Mtu Anacho!!!
Wote tumepewa muda sawa
Kuna kitu kimoja pekee hapa duniani ambacho Mungu amempa kila mtu bila upendeleo ni muda. Kufanikiwa au kutokufanikiwa kwa mtu kunategemea sana namna anavyotumia muda wake.
Tajiri namba moja duniani na masikini anaelala kwenye mitaro wote wamepewa muda sawa sawa saa 24 kwa siku hakuna aliyezidishiwa hata sekunde moja au kupewa kwa upungufu. Muda ni kitu kipo tu na wala hakiko ndani ya uwezo wetu.
Karibu tena msomaji wetu wa mtandao huu wa maisha ni fursa. Leo tutajikita zaidi kwenye mada ambayo nimeipa kichwa “KITU HIKI KILA MTU ANACHO” Nashukuru kwa kuendelea kutuamini na kufuatilia kazi zetu,kwani bila wewe kazi yetu haina maana.
Watu wengi wanaishi bila kuzingatia ukweli huu na matokeo yake wameharibu na kupoteza muda mwingi katika maisha yao ambao hawawezi kuonyesha matokeo yanayolingana na muda wao walioishi hapa duniani.
Muda hauwezi kusimama wala huwezi kuzuia siku ishiishe kwa namna yoyote ile,unachotakiwa kufanya ili muda uwe upande wako ni kuhakikisha unapanga namna ya kuutumia muda wako uliopewa na Mungu kwa ufanisi ili mwisho wa siku uwe na kitu cha kuonyesha.
Umewahi kumwambia mtu au kusikia mtu anasema siku yangu imeharibika? Siku au muda ulioharibika ni ule muda ambao umeuruhusu upite bila kutumika kukusaidia kutimiza kusudi la kuwepo kwako hapa duniani.
Watu wengi wanajua kuwa muda ni mali na zaidi ya hapo tena wanafahamu wanachopaswa kufanya ili kupanga njia nzuri ya kutumia muda wao lakini ukweli ni kwamba watu wengi hawapangi kutumia kile wanachojua kuboresha maisha yao.
Kwa sababu kwa asili mwili hautaki kuwekewa utaratibu wa kuubana,mwili unapenda uhuru ambao utamwezesha mtu kufanya chochote anachotaka kufanya ndiyo maana kubadilisha tabia inahitaji sana mtu kumaaanisha.
Kwa kuwa kujua njia bila kuitumia haitoshi kukufikisha kule unakotaka kufika ndio maana watu wengi wananunua kalenda kwa ajili ya kuwasaidia kupanga siku lakini wanaishia kuwa nazo mezani mwezi mapaka mwaka unaisha.
Tunapaswa kuwa waanglifu kuhakikisha tunapanga matumizi ya muda wetu kabla ya kuanza kutumia kiholela maana siku huanza kuharibika asubuhi na hizo asubuhi zikiwa nyingi ndizo zinazotengeneza mwezi ulioharibika na kisha mwaka ulioharibika.
Kabla sijakuomba tuingie kwenye zoezi naomba chukua kalenda yako ya mwaka jana pitia ukurasa baada ya ukurasa mwezi baada ya mwezi uone kama kurasa zote zimejaa. Ingawa kujaza kurasa siyo dalili ya kukuonyesha kuwa umetekeleza lakini ni dalili ambayo inaonyesha angalau unajua kile unachopaswa kufanya.
Kutokujaza kalenda ni dalili kwamba unajua matumizi ya kalenda lakini hujui umuhimu wa kuitumia na madhara ya kutokutumia kalenda.Ungejua na ukawa na sababu nzito nyuma yako hungeacha kuitumia kikamilfu.
Nataka nikuombe ufanye zoezi hili muhimu kama una kalenda ambayo ulinunua kwa ajili ya kukusaidia kupanga siku au unatumia aina fulani ya daftari kupanga matumizi ya muda wako. Sasa leo ni tarehe 7.1.2019 hebu fungua kama mpaka jana umejaza tarehe ya jana na zingine zote zilizotangulia.
Utagundua tayari umekwishauanza mwaka kwa kuendekeza na kuruhusu uharibifu wa muda wako ufanyike chini ya usimamizi wako na hapo unaelekea kuanza kutengeneza mwezi ulioharibika sio ajabu ukafuzu tunapomaliza mwaka ukawa umefaulu kuharibu mwaka bila kutaka.
SASA UNAWEZAJE KUTUMIA MUDA WAKO VIZURI?
Kuwa na kalenda bila kuitumia ni sawa sawa na kutokuwa na kalenda kabisa wala haileti maana na madhara yoyote chanya katika maisha ya wewe unayemiliki kalenda. Lengo la kuwa na kalenda ni ili ikusaidie kupanga namna nzuri ya kutumia muda wako.
1. Andaa kalenda au daftari
Uwe na kalenda au daftari ambalo utalitumia kupanga namna ya kutumia muda wako vizuri kila siku na kuhakikisha hakuna siku inapita bila kutumia hilo daftari au kalenda.
2. Panga siku yako mapema
Njia nzuri ya kupanga siku ni kuhakikisha kila siku kabla hujalala unapata muda wa kufanya tathmini ya namna ulivyotumia muda wako. Mahali ambapo hukufanya vizuri unaweka mkakati wa kuboresha kesho.Tathmini itakuongoza kuweza kupanga siku yako ya kesho kwa kuzingatia hali halisi.
3. Ishi ulichojipangia usichokipamgia acha
Watu wengi wanaweza kupanga lakini kuishi kile wanachopanga ni changamoto. Haina maana kuweka kwenye karatasi namna utakavyotumia muda wako na kuishia hapo bila kuchukua hatua kuweka kwenye matendo.
Ni matarajio yangu kwamba utafanya umauzi na kuumanisha kuufanya mwaka 2019 kuwa ni mwaka wa mafanikio na mapinduzi makubwa katika maisha yako. Kumbuka muda hauwezi kukusubiri wenyewe utapita iwe umejiandaa au hukujindaa.
Naamini utakuwa umepata kitu kingine kupitia makala hii fupi. Ukiwa na uhitaji wowote au ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasiliana nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini.Aidha kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno au whatsapp au piga simu au email tutapokea na kurudi kwako mapema kadri itakavyowezekana.
Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale
Simu +255784503076
Email:maishanifursa2017@gmail.com