Namna Ya Kupata Fursa Ya Biashara

Watu wengi wanatamani kuwa wajasiliamali lakini changamoto kubwa inayowakwamisha ni kutokua na uwezo wa kubuni wazo la biashara.Watu wanaofanikiwa kila watakakokwenda ni wale wenye uwezo wa kutazama tofauti na watu wengine wanavyotazama na kupata fursa katikati ya kile wengine wanachoita matatizo.

Kwa nini mtu mmoja ana uwezo wa kuona fursa na kubuni biashara moja baada ya nyingine kila anakokwenda,lakini mwingine hawezi kubuni kitu chochote zaidi ya kuiga watu wengine wanachofanya? Nini kinachowatofautisha watu hawa wawili?

Karibu tena katika makala zetu za kujenga katika mtandao wa www.maishanifursa.com  .Kwanza nikushukuru sana kwa kuendelea kutuamini na kufuatilia kazi zetu. Kazi hii ina maana tu kwa sababu wewe upo. Kama ni mara yako ya kwanza kutembelea mtandao wetu,nikukaribishe kwa mikono miwili na kuahidi kuwa hutakaa ujute kuufahamu mtandao huu. 

Leo nataka tutafakari pamoja juu ya mada niliyoipa kichwa “Namna ya kupata fursa ya Biashara”eneo ambalo naamini wengi wetu tunahangaika na wapo ambao wamefikia mahali pa kuua ndoto zao za kuwa wajasiliamali kwa kushindwa tu kujua mahali pa kuanzia.

Zipo fursa tatu ambazo Mungu amempa kila binadamu aliyeko chini ya jua kuzitumia kwa ajili ya kufanya chochote ambacho ataweza kufanya kugusa maisha yake binafsi na ya watu wengine.

1.Muda: Madhari unaishi na unaweza kusoma makala hii ukaelewa bila kujali hali yako, basi wewe ni miongoni mwa watu waliopewa na Mungu hii zawadi ya muda uitumie unavyotaka.Jambo la muhimu kukumbuka ni kwamba muda kwetu binadamu una ukomo siyo kitu cha kudumu milele.Ukijua hivyo basi haitoshi tu kujua hakikisha unaishi kana kwamba utaondoka kesho na je ukiondoka utaacha nini nyuma yako?

2. Uwezo: Kila mtu amewekewa namna fulani ya uwezo ndani yake ambao akiutumia vizuri kwa uaminifu, basi atafanya chochote anachotaka kufanya,bila kukwazwa na kitu chochote.Uwezo ulio ndani ya mwanadamu ni mkubwa kuliko vile unavyoweza kiviita vikwazo au matatizo . Ni uwezo unaomtofautisha mtu mmoja na mwingine.

Mtu mwenye uwezo ndani yake hafungwi na mipaka yoyote katika maisha yake,kila kinachokuja mbele yake anapata namna ya kutoka na kufanyika fursa.Mtazamo wa mtu anayejitambua kuwa ana uwezo ni tofauti kabisa na watu wengine wanaojiona hawana uwezo. Kwa kifupi hakuna mtu asiye na uwezo kinachokosekana ni taarifa na kutojikubali kwamba ana uwezo.

3.Ubunifu: Ubunifu ni kitu cha pekee kilicho ndani ya uwezo wa mtu. Kila mtu amepewa uwezo wa namna fulani ndani mwake kubuni.Kukosekana kwa ubunifu ndicho chanzo cha watu wengi kuanzisha biashara kwa kuiga watu wanachofanya na matokeo yake biashara nyingi zinahangaika na kushindwa kufanya vizuri.

Ubunifu unahitajika katika mazingira na kazi yoyote.Katika uongozi na utawala,katika biashara,katika ufundi na mazingira yote ya kazi.Ukikuta watu wanaofanikiwa kufanya vitu vya pekee fuatilia utagundua kuwa ni wale wanaofungua na kutumia hazina iliyo katika masanduku yao ya ubunufu.

Jinsi ya kupata fursa ya biashara.

Baada ya utangulizi hapo juu twende kwenye lengo.Namna ya kupata fursa ya biashara ni rahisi kuliko unavyoweza kufikiri ukizingatia vitu vitatu tuilivyofafanua hapo juu. Labda niweke tahadhari kwamba si rahisi kwa kila mtu,ila ni rahisi kwa anayejua kanuni kwa sababu ipo kanuni rahisi ya kufuata kukuwezesha kupata fursa ya biashara.

Fuatilia malalamiko.

Fatilia watu wanakopata huduma wanalalamikia nini? na wewe usijiweke pembeni uwe miongoni mwa wale wanaolalamika. Kama kuna mahali unakwenda kupata huduma halafu wewe mwenyewe unajikuta katika hali fulani ya kulalamika kutokana ama na huduma mbovu ulizopata,au kasoro ulizoona katika biashara au huduma ile;basi uwe mwangalifu usije ukajikuta unaishia kulalamika t uko jirani na fursa.

Malalamiko mara nyingi huwa ni lugha au ushuri ambao wateja au watumiaji wa huduma huwa wanajaribu kutuma kwa njia isiyo rasmi juu ya namna ambavyo hawaridhishwi ama na huduma au bidhaa waliyolipia. Mjasiliamali mbunifu akisikia malalamiko ya wateja anajua kuwa kuna hitaji halijatimizwa. Si unajua biashara ni suluhu ya mahitaji fulani mahala fulani.

Wapo watu wengi wanaolalamika na kuishia kulalamika tu. Jitofautishe na watu wengine.Angalia hadi nyuma ya pazia ili uone kama ipo fursa yoyote ndani ya ule udhaifu. Kwa kifupi udhaifu unaoona kwa watu wengine,huo ndio wito wako unaoweza kukupa wazo la biashara au huduma. Unajuaje kama ni wewe peke yako unaeona udhaifu huo?

Fuatilia,jifunze huku ukijiuliza ni kitu gani unaweza kufanya kuanzisha biashara au huduma itakayokuja na majibu ya changamoto nyingi ulizoona na hata wengine walizoona.Ukiwa makini utakuta unabuni wazo jipya la biashara au huduma ambayo itachukua muda watu wengine kuiga na hata wakiiga watahangaika sana kushindana na wewe kwa sababu wewe ni mbunifu siyo muigizaji mawazo ya watu.Kumbuka ni vigumu sana mtu kubuni kitu ambacho hakijawahi kufanyika mahali popote,ila sanaa ni ule ufundi wa kujitofautisha na watu wengine.

Kumbuka ile tu kuwa katika hali ya uzima na afya maisha ni fursa Mungu aliyotupa na hatuna kisingizio chochote kushindwa kufanya chochote ambacho ungependa kufanya.

Naamini utakuwa umepata kitu kupitia makala makala hii fupi. Kama utakuwa na uhitaji wowote au ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasiliana nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini.Aidha kwa email,kutuma ujumbe mfupi wa maneno au whatsapp au piga simu. June 27/2017

Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale

+255784503076-habarilulale@gmail.com


Previous
Previous

Kitu Hiki Kila Mtu Anacho!!!

Next
Next

Jifunze Kusema Hapana Itakusaidia…