Muhimu Ni Mwisho Siyo Mwanzo!
Muhimu Mwisho Siyo Mwanzo
Alikuwa ni fundi mwashi mzuri na maarufu sana wa wakati wake. Kutokana na ustadi na umaridadi wa kazi yake,alifanya kazi ya ujenzi mpaka akawa sababu ya mtu aliyekuwa amemwajiri kutajirika kutokana na kukubalika kwa kazi zake.
Alikuwa na sababu ya kuwa maarufu klutokana na kazi hiyo ambayo alifanya tangu enzi za ujana wake hakuwa kufanya kazi nyingine maisha yake yote mpaka anafikia sasa hatua ya uzee na kustaafu kazi kutoka kazi yake hiyo iliyomlea kipindi chote cha uhai wake.
Kuna mafundi wengi vijana na watu wazima waliopita mikononi mwake ambao wale waliotimu kufuata maelekezo yake kwa kufanya kazi kwa ubora wa wa hali ya juu, uaminifu na kujituma ilimtofautisha sana na mafundi wengi wa aina yake kijijini kwao na maeneo yaliyozunguka kijiji chao.
Kama unavyojua wakati wa kustaafu ulipofika mzee Matokeo aliomba sasa apumzike, kwa kuwa alikuwa ameitumikia kampuni hiyo kwa zaidi ya miaka 30 mfululizo, kwa uaminifu na ufanisi mkubwa. Tajiri yake alikubali lakini hakujua ni zawadi gani angempa mzee Matokeo ambaye aliipandisha sana kampuni hiyo kibiashara.
Karibu tena katika makala zetu za kujenga katika mtandao wa maishanifursa.com. Kwanza nikushukuru sana kwa kuendelea kutuamini na kufuatilia kazi zetu. Kazi hii ina maana tu kwa sababu wewe upo. Kama ni mara yako ya kwanza kusoma makala zetu nikukaribishe kwa mikono miwili na kuahidi kuwa hutakaa ujute kuufahamu mtandao huu.
Hujawahi kufanyiwa kitu na mtu mpaka ukajikuta unashindwa kupata kitu chochote cha kumpa kuonyesha shukrani kwa jambo jema alilokufanyia mtu huyo katika maisha? Hiyo ndiyo hali aliyokutana nayo tajiri yake mzee Matokeo ambaye alikuwa anamiliki kampuni ya biashara ya ujenzi majumba na kuuza ardhi.
Wakati akiendelea kufikiria angemfanyia nini mzee Matokeo kama shukrani kwa mfanyakazi wake huyo,mwenye juhudi kubwa na mwaminifu alimwomba mzee Matola amjengee nyumba moja ya mwisho ambayo itakuwa ni kama ukumbusho kwenye kampuni yake, na mzee Matokeo aliona ni jambo la fahari kulitekeleza.
Alionyeshwa uwanja mahali alipanga nyumba ijengwe na kontena la futi 40 lililokuwa limejaa vifaa vya ujenzi vyote vilivyohitajika. Mzee Matokeo alianza kazi ya ujenzi lakini tofauti na jinsi alivyokuwa amezoeleka kufanya, safari hii alibadilika kabisa.Mahali ambapo alipewa mifuko 400 ya saruji alitumia 150 na 250 akapeleka alikojua yeye.Alifanya hivyo karibu kwa kila vifaa isipokuwa bati ndiyo alishindwa kuchakachua.
Jengo lilikamilika lakini kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30 mzee Matokeo alichofanya kazi kwenye kampuni hiyo ya ujenzi,alijenga nyumba dhaifu kuliko nyumba zote ambazo aliwahi kujenga na ilimshangaza kila mtu.
Wakati wa kukabidhi jengo kwa aliyempa kazi,tajiri yake alikuja akalitazama jengo lenyewe akamtazama mzee Matokeo usoni,machozi yakamlengalenga kwani hakuwa na taarifa kama huo ndio ungekuwa mtindo wa mzee Matokeo kuagana na yeye.
“Mzee Matokeo ninajua kila kilichoendelea hapa site na jinsi ambavyo ulikuwa unahamaisha vifaa hapa kupeleka ulikokuwa unajua wewe mwenyewe,sikutegemea kwani kwa kweli mzee ninakuamini sana na ndiyo maana muda mwingi wewe ulikuwa unafanya kazi zako bila kuwepo usimamizi wangu wa karibu,sasa tulipofika ni jambo ambalo sikulitegemea” alilalamika tajiri wa mzee Matokeo.
“Basi babangu nashukuru sana nimekagua na naomba kesho uje na familia yako nina jambo nataka kuongea na wewe ukiwa pamoja na familia yako” waliachana na kusubiri kesho yake.
Kesho yake mzee Matokeo alipofika ofisini walikaribishwa na kuingia ofisini kwa mkurugenzi na kusaini kitabu cha wageni;kisha walielekezwa kwenye eneo la tukio ambapo mbele ya ile nyumba aliyojenga kulikuwa na hema kubwa ndani mwake kukiwa na viti.Ilikuwa ni sherehe fupi ya kumwaga mtumishi wa muda mrefu wa kampuni hiyo mzee Matokeo ambaye ametumikia kampuni kwa zaidi ya miaka 30 kama fundi.
Mwisho wa sherehe mkurugenzi wa kampuni alimkabidhi mzee Matokeo funguo za nyumba aliyokuwa amejenga ambayo alisema ni zawadi ya kampuni kwa mzee huyo kuenzi utumishi wake uliotukuka wa muda mrefu kwenye kampuni.Sitaki kusimulia hapo nini kilitokea kwa mzee Matokeo zaidi ya ukweli tu kwamba alitamani siku zirudi nyuma ili aanze upya kwani hakutegemea.
Lipo funzo fupi katika kisa hiki ambacho nilipata bahati ya kusimuliwa na rafiki yangu mmoja.Angalia sana unavyoishi na kuhakikisha unamaliza kwa ushindi kama ulivyoanza kwani,watu hawataangalia ulivyoanza ila watakachotazama ni ulivyomaliza.
Lipo funzo katika kisa hiki ambacho nilisimuliwa na rafiki yangu.Fanya kila kitu kwa haki bila kujali mnufaika ni wewe au ni mtu mwingine zaidi.Cha muhimu ukipata nafasi ya kufanya kitu,basi fanya kama ambavyo ungetamani wewe watu wakufanyie.Kama unauza hakikisha mteja anapata bidhaa inayolingana na thamani aliyolipia,usipunje mtu kwa sababu tu yeye hajui hapana,lazima kuwa mawakili waaminifu.
Kama umekubaia na mtu kufanya kazi ambayo ungepaswa kulipwa shs milioni 3 lakini mkakubaliana kulipwa milioni moja,basi huduma yako hakikisha inakuwa ya thamani ya shilingi milioni 3 na siyo milioni 1 kwani ulikubali mwenyewe.
Siku zote tumia kanuni ya kulipa thamani ya zaidi ya kile ulicholipwa kulikomkutamani kupata faida bila kuangalia thamani unayoongeza kwa binadamu wanaokuzunguka. Dunia tunayoishi wapo binadamua wanatafutwa kila wanakokwenda na wengine wanaombewa watoke kulingana na mambo ya ajabu ambayo wamefanya kwa binadamu wenzao.
Masha ni fursa bila mipaka na dunia ina njaa na kiu ya watu waaminifu ambao uaminifu wao hautenganishwi na hali yoyote,iwe wana kitu au hawana,au wawe katika hali ya namna yoyote.Ukiamua kuwa mtu mwaminifu hakikisha unabaki kuwa mwaminifu katika mazimgira yote bila kujali unapita katika kipindi cha namna gani.
Naamini utakuwa umepata kitu kupitia makala kitu kingine kupitia makala hii fupi. Kama utakuwa na uhitaji wowote au ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasili nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini.Aidha kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno au whatsapp au piga simu hapo chini. June 19,2017
Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale
WhatsApp No. +255784503076-|
Email: Maishanifursa2017@gmail.com