Maisha Ni Mradi Wako Mwenyewe!
Picha kwa msaada wa teknolojia
“Maisha ni mradi wa kufanya wewe mwenyewe (life is a do yourself project)” ni msemo na nukuu ya Napolion Hill kupitia kitabu chake maarufu cha Think and Grow Rich alipokuwa anasisitiza juu ya umuhimu wa kila binadamu kutimiza wajibu wake kuhakikisha anafikia kusudi la kuwepo kwake hapa duniani.
Karibu tena msomaji wa makala zetu kwenye mtandao wetu. Leo nimechagua kukushirikisha mada inayoitwa “Maisha ni mradi wako mwenyewe” na nikushukuru tu kwa muda wako uliotenga uendelea kufuatilia mada hizi. Nathamini sana mchango wako huo.
Watu wengi wanajua umuhimu wa muda katika maisha na wengine wanaishi bila kuwa na taarifa kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya muda na maisha.Hivi ni vitu vinavyotegemeana sana. Pasipo muda hakuna maisha na hakuna muda kwa mtu kama hakuna maisha.Huwezi kuvitenganisha hivi vitu viwili kamwe.
Kuna misemo mingi ambayo imetumiwa na watu tangu zama za mababu kuonyesha umuhimu wa muda katika maisha ya mwanadamu. Misemo kama muda ni mali inaonyesha kwa kiasi gani watu wanajaribu kusisitiza thamani ya muda pale wanapolinganisha muda kuwa kama kitu cha thamani sawa na pesa au mali.
Licha ya watu wengi kukiri kwa vinywa vyao ya kwamba muda ni kitu cha thamani lakini ukweli ni kwamba ni watu wachache sana wanaoweka imani hiyo katika vitendo kwa hiyo wanatamka kwa vinywa lakini mioyoni mwao hawaamini kabisa huo ukweli.
MAISHA NI NINI?
Maisha ni kile kipindi mtu anachoishi duniani kati ya kuzaliwa na kufa ndio msimu unaoitwa maisha. Maisha siyo kitu cha kudumu ni kitu cha muda,ingawa watu wengi wanatamani kuishi maisha marefu hapa duniani ukweli ni kwamba maisha ni kipindi kifupi sana cha mwanadamu kuishi hapa duniani.
Toafauti na wanyama na viumbe wengine binadamu amepewa maisha akiwa amebeba kusudi maalum la kutimiza hapa duniani kwa muda maalum. Maisha ni kitu kilichofungwa katika uwezo wa Mungu mwenyewe na hakuna binadamu anayejua kuwa ataishi kwa muda gani duniani.
Kila siku unapaswa kutekeleza majukumu yako kwa uaminifu huku ukiwa unajua kuwa wakati wowote Mungu atakaotaka muda wako kuishi duniani unaweza kufikia ukingoni.Ni hatari sana kufanya kama wanavyofanya wengi kuahirisha kufanya mambo kwa kutegemea kuwa pengine utafanya kesho,kesho ina mambo yake na pia kesho siyo yako.
Unapaswa kumshukuru Mungu kwa kutimiza wajibu wako hapa duniani kwa uaminifu,kwa sababu kuwepo kwako mpaka leo iko ndani ya mapenzi yake na hakukuweka bure lipo kusudi la kutekeleza ndani ya hiyo zawadi ya muda uliyopewa
Kumbuka kuna walioona jua siku moja wakafa,wapo walioishi miezi kadhaa,wapo walioishi mwaka mmoja,wapo walioishi miaka kumi,ishirini,miaka hamsini,themanini,mia wakamaliza kipindi cha kuishi kwao hapa duniani.
MRADI NI NINI?
Mradi ni zile shughuli maalum ulizopanga kufanya katika kipindi maalum na shughuli hizo lazima ziwe ni zile zinazosaidia kutimiza kusudi la kuwepo kwako hapa duniani siyo shughuli mradi uonekanane unafanya shughuli hapana.
Muda ni raslimali muhimu ambayo Mungu amempa mwanadamu ili kumwezesha kutekeleza mradi au shughuli anazopaswa kufanya katika kipindi chote cha nihai wake. Muda ni kitu cha thamani kwa hiyo na muda wa mtu una mwanzo na kama una mwanzo lazima pia uwe na mwisho.
Kama muda ni kitu cha thamani basi mwanadamu unapaswa kupanga vizuri namna ya kuutumia kulingana na maono na kusudi lililo ndani mwako ili kuhakikisha unakuwa wakili mwaminifu kwa raslimali muda uliyopewa na Mungu.
Ukiuliza watu wengi ni kitu gani ambacho mwanadamu anapaswa kukiogopa sana kuliko vitu vyote,bila shaka jibu linaweza kuwa kifo! Ukweli ni kwamba kitu ambacho mwanadamu anapaswa kukiogopa kuishi bila kujua unakoelekea.
Kwa nini muda ni muhimu kwa maisha ya mwanadamu? Muda ni muhimu kwa sababu ili uweze kutimiza kusudi la kuwepo kwako hapa duniani unapaswa kuwa na muda bila muda hakuna chochote unachoweza kufanya. Muda ni kitu chamsimu cha thamani sana kwa hiyo binadamu unapaswa kukichukulia kwa uzito na mtazamo tofauti kabisa.
Binadamu anagawanyika katika misimu minne muhimu. Msimu au kipindi cha utoto,kipindi cha ujana,kipindi cha utu uzima na kipindi cha uzee. Katika vipindi hivyo vyote msimu wa ujana ndio msimu muhimu sana kuliko misimu mingine yote kwani wakati huo una nguvu ya kufanya chochote unachotaka kufanya.Kipindi cha utu uzima tayari unaanza kukabiliwa na vikwazo yapo mambo ambayo unataka kufanya lakini mwili unaleta vikwazo.Kipindi cha uzee hapo usisahu huo ni msimu wa lala salama ambao unabaki kutamani kufanya bila kuwa na uwezo ule uliokuwa nao wakati wa msimu wa ujana.
Kila jambo linapaswa kufanyika kwa wakati kwani upo wakati binadamu utakuwa unaweza kufanya jambo fulani na upo wakati utakuwa huwezi kufanya jambo kutegemeana na wakati.
Watu wengi wanapenda kuwa waangalifu kupanga mambo ya kitambo watakula nini leo,kesho,wiki hii na kusahau kupanga mambo muhimu katika maisha kama namna bora ya kutumia muda kama raslimali muhimu wakidhani kwamba wanao muda mwingi wa kuishi holela.
Kila dakika inayopita maishani mwako haipaswi kupotea.
Hebu tuchukulie mfano huu halisi katika maisha:wastani wa mtanzania kuishi kwa hekima ya kibinadamu inakadiriwa kuwa karibu ni miaka 60 sasa na wastani wa mtu kuishi kwa mujibu wa hekima ya neno la Mungu ni miaka 70 na iwapo tuna nguvu ni miaka 80.
Kati ya kuzaliwa kusoma hadi kufanya kazi hadi kustaafu binadamu wa Tanzania ametengewa miaka 60 halafu anastaafu kufanya kazi. Mpaka hapo utaona jinsi gani muda wa kusihi hapa duniani ulivyo mfupi.
Kati ya miaka hiyo 60 kuna miaka ya utoto 17 ambayo utakuwa bado unaishi kwa wazazi hujajitegemea ukisubiri utimize miaka 18 ingawa kwa mazingira yetu ni wachache sana wanaofaulu kujitegemea wakiwa na umri wa miaka 18.
Kama umepata mpenyo wa kuendelea na masomo ya juu tuseme utatumia miaka 24 hadi kumaliza shahada yako ya kwanza ya chuo kikuu ndipo sasa uanze kujitegemea. Sasa katika miaka 60 hiyo ya maisha utakuwa umebakiwa na miaka 36 tu ya kufanya kazi.
Tuseme umepata ajira kama mtazamo wako ni kuajiriwa maana si kila mtu anataka kuajiriwa basi utafanya kazi huku kadri siku zinavyokwenda na wewe thamani yako inapungua polepole mpaka utakapofikisha umri wa miaka 55 kutagundua kuna dirisha dogo limefunguliwa kwa ajili ya wale wanaotaka kustaafu kwa hiari wafanye hivyo.
Inapogonga tu miaka 60 hapo mlango mkubwa unafunguliwa wa wewe kuatakiwa kuondoka kwa mujibu wa sheria,kwa lugha rahisi mimi hupenda kuita unatakiwa kustaafu utake usitake lazima.Ingawa moyoni ungetamani kuendelea kuwepo kazini lakini ukweli ni kwamba hauhitajiki tena maana umetumika mpaka nguvu zimekwisha unatakiwa ulipwe kile kinachoitwa kiinua mgongo halafu uondoke ukajisikilizie ukisubiri siku za kumaliza mkataba wako duniani zitimie.
Siku moja kila binadamu amepewa saa 24 na mwaka mzima wenye siku 360 kila binadamu amepewa saa 8640 na kwa miaka 60 mtanzania ana saa 518,400. Hizo ni jumla ya saa ambazo amepewa kutumia katika kipindi chote cha kuzaliwa kusoma na kufanya kazi ndani ya miaka hiyo 60.
Miaka yako 24 kuzaliwa hadi kusoma mpaka shahada ya kwanza ya chuo kikuu tayari umekwishatumia saa 207,360 na hapo unabakiwa na saa 311,040 karibu sawa na nusu ya muda wako wa kufanya kazi. Hakuna binadamu aliyefaulu kutumia saa zote 24 kwa siku kuna mgawanyo Mungu alikwishaweka wa namna ya kutumia.
Nchini Tanzania kama umeajiriwa unaingia kazini saa 1:30 na kuwepo kazini mpaka saa 9:30 na kufanya saa za kuwa kazini kuwa ni saa 8 ingawa kuna muda wa kupumzika mchana kwa ajili ya chakula.Utagundua kwamba mtanzania aliyeajiriwa anafanya kazi kwa saa 8 kwa siku yenye saa 24 ,sawa na saa 240 kwa mwezi,sawa na saa 2880 kwa mwaka na kufanya jumla ya saa 103,680 kwa kipindi chote cha kudumu kwenye ajira cha miaka 36 kabla ya kustaafu.
Kwa kawaida wanasema binadamu mtu mzima anatakiwa kupumzika au kulala saa 8 kila siku hivyo kutakuwa na saa zingine 103,680 za kulala na hivyo muda wa kufanya kazi na ule wa kulala unakuwa ni saa 201,760. Saa zingine 103,680 ni zile ambazo ungeweza kutumia kwa kazi nyingine lakini watu wengi hupoteza muda huu kwa kulala zaidi au kufanya mambo ambayo hayana tija yoyote katika maisha.
Mpaka hapo utaona namna ambavyo muda wa kufanya kazi ni mdogo kuliko watu wengi wanavyodhani kwani katika umri uliotengwa wa mtanzania kuishi wa miaka 60 ambapo ni jumla ya saa 518,400 ni saa 103,680 tu za kufanya kazi.
Mpaka hapo kama tumekwenda pamoja vizuri kupitia makala hii nitakuwa nimekusaidia kuweza kubadili jinsi unavyochukulia maisha na mshirika wake wa karibu muda kuwa binadamu siyo mitu cha kudumu tunaishi kwa msimu mfupi kwa kazi maalum.
Naamini kuna kitu utakuwa umejifunza kupitia Makala hii fupi ya “Maisha ni mradi wako mwenyewe”. Ikiwa ungependa kusoma zaidi makala zetu endela kutembelea mtandao wetu. Na kama ungependa kuingia kwa undani katika mada hizi kwa maswali au kujifunza zaidi usisite kuwasiliana nasi kwa kutuma ujumbe mfupi wa simu,kupiga au whatsApp kupitia simu hapo chini.
Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale
WhatsApp +255784503076
Email:maishanifursa2017@gmail.com