Maneno Bila Matendo Haitoshi!

“Nitalima maharage mengi sana na mahindi katika shamba hili.Siku ya kuuza mazao yangu hakuna mkulima mwingine atakayepata nafasi ya kuuza,kuanzia asubuhi mpaka muda wa kufunga soko nitauza mazao yangu tu” alisisitiza

Mategemeo aliachiwa eneo kubwa la shamba la urithi na baba yake kabla hajafariki,ambaye alikuwa mkulima mkubwa katika eneo hilo lenye maji na rutuba ya kutosha kulima chochote ambacho angetaka kulima kikastawi.

Karibu tena msomaji wetu wa mtandao huu wa maisha ni fursa. Leo tutajikita zaidi kwenye mada ambayo nimeipa kichwa “Maneno Bila Matendo Haitoshi.” Nashukuru kwa kuendelea kutuamini na kufuatilia kazi zetu,kwani bila wewe kazi yetu haina maana. 

Kabla ya kifo cha baba yake mahali pale palikuwa kimbilio la watu kwa ajili ya watu kuondokana na tatizo la njaa. Alikuwa ni mzuri sana kupanga mipango ambayo hakuwahi kuitekeleza. Mara nyingi alikwenda kusimama mbele ya lile shamba na kutamka yale aliyokuwa anafikri yangemsaidia kutimiza azima yake ya kuwa mkulima mkubwa.    

“Nitalima maharage mengi sana na mahindi katika shamba hili. Siku ya kuuza mazao yangu hakuna mkulima mwingine atakayepata nafasi ya kuuza, kuanzia asubuhi mpaka muda wa kufunga soko nitauza mazao yangu tu” alisisitiza. Baada ya miaka mitatu nitakuwa mkulima mkubwa anayemiliki vitendea kazi vya kisasa vya kilimo kwa ajili ya kunisaidia kulima kilimo cha kisasa” Alifikiri na kujisemea karibu kila siku namna hiyo, lakini alipohesabu gharama alijikuta anaishiwa nguvu za kuanza kutekeleza kile alichoamini katika moyo wake kuwa ni wazo sahihi la kumtofautisha na wakulima wengine.

Mara nyingi kila alipotaka kuchukua hatua alijikuta anaona mbele yake mlima mkubwa ambao karibu hauwezekani kuupanda na kuishia kukata tamaa na kujipa matumaini ya kusogeza muda mbele kutekeleza kile alichokuwa anaona ndani mwake.

Ndani mwake alikuwa na maono na picha kubwa ya namna alivyotaka kuwa mkulima mkubwa na maisha yake yangegusa maisha ya watu wengine katika kijiji chake, kutokana na kazi kubwa ambayo angekuwa anafanya katika shamba lake la mfano wa kuigwa na watu wengi lakini hakuwa na ujasiri wa kutosha kuanza kutekeleza. 

Siku moja alikuwa amesimama katikati ya shamba lake kubwa akiangalia mazao yake alivyokuwa yamependeza. Haikuwa mchezo ndani ya ekari 100 amelima mahindi, maharage,ufuta na mtama.shamba lake lilikuwa na wafanyakazi zaidi ya 20 waliokuwa wamegawana majukumu mbalimbali.

Alikuwa amefanikiwa kununua zana kaza za kisasa za kilimo ikiwemo matrekta mawili. Watu kutoka maeneo mbalimbali walikuja kujifunza katika shamba lake namna ya kuendesha kilimo bora cha kisasa. Kumbe ilikuwa ni tukio la kuota alipokuwa usingizini. Ule mkanda uliokuwa kichwani mwake ulikuwa unacheza sasa usiku kucha kumbukumbu za matukio ya mchana kutwa. 

Alifikia hatua ya kushirikisha watu wengine nia aliyokuwa nayo kuendesha kilimo kikubwa cha kisasa katika shamba lake kubwa aliloachiwa urithi na marehemu baba yake.Alieleza jinsi alivyotamani awe mkulima wa kisasa ambaye atamiliki maghala makubwa ya zao la mahindi na maharage kikjijini kwake. 

Wengine walimtia moyo na wengine walimkatisha tamaa kwamba jambo hilo ni ndoto kubwa sana kuweza kutekelezwa na yeye ambaye hata hakuwa na uzoefu wa aina yoyote katika maisha.Walimwambia alihitaji kuanza kidogo kidogo na wengine walimtishia kuwa soko la vitu anavyotaka kulima halipo.

Miaka iliendelea kupita na kufikia sasa umri ambao alikuwa hawezi tena kukimbia kimbia huku na huko kutokana na umri wake kwenda mbali. Alikuwa hawezi tena kuwaza na kutekeleza kitu chochote. Mwisho alikufa bila ya kuwahi kuwa mkulima mkubwa kama alivyokusudia. 

Ni mawazo mangapi umekuwa ukiahirisha kutekeleza kila siku na kujikuta unashindwa kutekeleza kitu chochote katika maisha yako. Tabia ya kuchelewa na kuahirisha mambo ni ugonjwa unaowasibu watu wengi katika maeneo mbalimbali. Mwenyenzi Mungu alipotuumba aliweka ndani mwetu uwezo wa kuumba na kutawala. Kuna uwezo mkubwa sana ndani ya mtu kuweza kuunda chochote ambacho angetaka kuunda.

Mawazo ni kama mama mjamzito ambaye anachukua mimba na kuilea hadi kufikia hatua ya mtoto kuzaliwa. Ni jambo la kusikitisha kama mama atachukua mimba na kubaki tu kuwa mjamzito bila kuiifungua mtoto! Hapo mategemeo hayatakuwa na maana yoyote.Au ni jambo mama kuharibu mimba kabla hata ya wakati wa kujifungua!

Kuwa na mategemeo na mawazo ya kufanya mradi fulani bila kufikia mahali pa kutekeleza ni sawa kabisa na mjamzito anayepata mimba na kushindwa akujifungua au kuharibu mimba. Ni mimba ngapi zimeharibika bila watoto kuzaliwa? Ni watoto wangapi wamekufa kabla ya kuzaliwa? Je ukiwekwa kundi la kina mama wabeba maono wauaji utakosekana kuwepo?  

Nataka nimalizie kwa kushauri kwamba kama unataka kufanya kitu chohote kusema tu hakutakusaidia kutekeleza chochote,lazima kutoka kwenye maneno na kuweka mawazo kwenye matendo.

Sisi sote tuna nafasi na nguvu ya kuchagua:kuchagua kuwa na malengo,kuchagua kuwa na chochote unachotaka kuwa nacho,kuchagua kuwa mtu fulani na lazima tuhesabu na kuingia gharama inayolingana na kile tunachotaka kuwa. 

Kumbuka ile tu kuwa katika hali ya uzima na afya maisha ni fursa Mungu aliyotupa na hatuna kisingizio chochote kushindwa kufanya chochote ambacho ungependa kufanya.

Naamini utakuwa umepata kitu kupitia makala hii fupi. Ukiwa na uhitaji wowote au ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasiliana nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini. Aidha kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno, whatsapp kupiga simu au kututumia barua pepe nasi tutarudi kwako mapema iwezekanavyo.

Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale

Simu:+255784503076                                 

Email:maishanifursa2017@gmail.com

Previous
Previous

Namna Nzuri Ya Kutafuta kazi

Next
Next

Muhimu Ni Mwisho Siyo Mwanzo!