“Unataka Kufanikiwa: Chagua Kipaumbele”

Kama kuna tabia inakwamisha watu wengi kufika katika kilele cha mafanikio wanayostahili duniani,basi ni tabia ya mtu kujaribu kufanya kila kitu katika maisha. Mtu kushindwa kujielekeza katika jambo moja na kujikuta anahangaikia kila fursa inayokuja mbele yake ni kikwazo kikubwa cha watu kufanikiwa.

Unakuta mtu leo anafanya shughuli fulani ya kumwingizia kipato na penguin amefanya kwa miaka kadhaa,hata kabla shughuli hiyo haijakaa vizuri unakuta kesho amerukia fursa nyingine mpya iliyojitokeza.

Unaweza kuona labda una uwezo wa kufanya vitu vingi na unayaona mafanikio lakini ukweli ni kwamba tumeumbwa kuwa wazuri katika jambo moja ambalo Mtu utajielekeza na kuwekeza nguvu,juhudi maarifa na raslimali zako nyingi kwa muda mrefu jambo hilo utafanikiwa.

Jambo ninalokushirikisha leo kwenye makala yangu siyo jambo geni tunaliishi kila siku na mifano imesheheni kila mahali hapa nchini na duniani kote. Umewahi kuona mtu anakuwa maarufu katika mchezo wa ngumi na wakati huo huo akawa maarufu katika mchezo wa masumbwi? Hata kama itatokea kuwa na kipaji cha kumudu michezo miwili au mitatu lazima katika hiyo mitatu utakuwepo mchezo mmoja ambao ukiupa kipaumbele basi utatoka kupitia hupo.

Mbwana Samata leo ni mchezaji maarufu katika mpira wa miguu,Mohamed Ally, Michael Tyson, Fransisi Cheka wamepata umaarufu hapa duniani kupitia mchezo wa masumbwi. Mifano ipo mingi ya watu maarufu hata wewe unaweza kuendeleza orodha hiyo lakini jambo la muhimu ni kwamba ukiwafuatilia watu maarufu wengi utakuta kuna kitu kimoja walichong’ang’ana nacho tangu wakiwa wadogo mpaka wanakuja kuwa na umaarufu wa kutosha kupitia kitu hicho walichoishi kwa muda mrefu.

Iko hivyo kwa taaluma unasoma mseto unapokuwa katika hatua za mwanzo lakini kadri unavyopanda juu kielimu kama unataka kuwa bingwa huwezi kuwa bingwa wa kila somo utachagua eneo moja (specializatiuon). Ndiyo maana huwezi kuwa bingwa wa magonjwa ya wanawake na watoto wakati huo huo ukawa bingwa au profesa uchumi. Fani ya uhandisi ni eneo pana huwezi mtu kuwa mhandisi wa kila kitu. Ukisikia fulani ni mwalimu wa ngazi yoyote uliza ni mwalimu wa kitu gani maana hawezi kuwa mwalimu wa kila kitu. Kuna mwalimu wa hesabu, mwalimu wa lugha,mwalimu wa maarifa, sayansi, jiografia n.k Ujumbe ni kwamba hauwezi kuwa mwalimu wa kila kitu.

Kama ambavyo mfumo wa elimu hauwezi kukupa nafasi kuwa profesa wa kila kitu ndivyo ilivyo pia mfumo wa maisha hauwezi kuruhusu ufanye kila kitu halafu uwe maarufu wa kila kitu au ufanikiwe.Kama unataka kufanikiwa katika eneo lolote maishani basi chagua eneo moja halafu ujielekeze katika hilo eneo utaona matunda.

Tofauti tu kati ya mfumo wa elimu na maisha ni kwamba ndivyo ilivyopangwa lazima uchague eneo moja unalotaka kubobea na katika maisha una hiari ya kuchagua kufanya kila kitu hakuna atakaekuzuia lakini mafanikio ujue utayasikia kwa mbali. Hata ukichagua kusoma kila kitu hakuna atakaekuzuia lakini hautakuwa bingwa wa kitu chochote.

Kwenye maisha kanuni muhimu ya kitu chochote utakachotaka kufanya ni kuchagua kitu ambacho katika maisha yako kitatumia muda wako mwingi maishani kukiishi na kutengeneza maisha kupitia hicho ulichochagua kuishi.

Kanuni iko hivyo iwe umechagua kuwa mwana michezo, mfanya biashara,mfanya kazi au mtaalam katika eneo au taaluma yoyote ya maisha. Kuna faida kubwa katika kuelekeza nguvu zako kwenye kitu kimoja unakipa muda wako mwingi maishani.

Watu wengi wamenaswa katika hili eneo na matokeo yake wamepoteza nafasi ya kuwa maarufu katika eneo lolote. Leo utakuta anafanya biashara hii, inakuja fursa ya kulima zao fulani anapunguza mtaji kwenye biashara yake na kuwekeza kwenye kilimo matokeo yake anajukuta hapati matokeo aliyotarajia katika kilimo na tayari amekwisha dhoofisha biashara haiendi kama ilivyokuwa inakwenda.

Kama kuna mahali tunahitaji kuwa waangalifu ni kwenye kufanya maamuzi ya nini cha kufanya katika maisha yako yote na kuacha mambo mengine yafanywe na watu wengine na wewe uwe mteja wao.

Katika chochote utakacho chagua mtu kuwa unahitaji elimu na uzoefu wa kutosha na elimu na ujuzi wa kweli hauji kwa kujaribu kufanya jambo kwa muda mfupi na kubadilisha kufanya shughuli nyingine. Katika maisha yawe ya kazi yoyote au biashara yana changamoto nyingi na kupitia hizo changamoto zinazoinuka katika maisha yako unapozivuka unatoka ukiwa umesheheni maarifa na ujuzi mpya wa namna ya kufanya vizuri zaidi.Kupanda na kushuka katika maisha kunakupa nafasi ya kujifunza na kuwa mtu bora zaidi katika eneo lako.

Angalia watu wengi waliofanikiwa katika biashara jifunze walianza na nini mpaka kufika mahali walipofika utakuta wanaenda kwa uangakifu sana wanapokua wanajaribu kukua kupitia eneo ambalo wameishi kwa muda mrefu kwa sababu ndilo eneo ambalo wana uzoefu wa kutosha. Mtu amefanya biashara ya kuuza mazao ya chakula anakwenda baada ya miaka anapanuka na kumiliki viwanda vya kuzalisha na kufungasha vyakula hajaenda mbali na eneo lake ameongeza tu mipaka katika hilo eneo lake.

Kadhalika mtu anaefanya biashara ya usafirishaji, kilimo, ufugaji utakuta mtu anapanuka kwa kuzingatia eneo ambalo ana uzoefu nalo na kukua polepole mwisho wa siku unakuta anabobea kuwa mtoa huduma mkubwa katika eneo ambalo amekaa muda mrefu

Kama wewe ni kijana iwe unaanza maisha au unataka kuanza maisha au umeshaanza maisha na umepata bahati ya kusoma makala hii niseme tu kwamba una bahati sana chagua kuchagua eneo ambalo utang’ang’ana nalo katika maisha kama unataka kufanikiwa haraka maishani. Achana na tabia ya kufanya kila kitu unaweza kuchelewa sana kifika kule unakostahili kufika. Dunia imejaa fursa nyingi kama ilivyo katika mchezo huwezi kuwa maarufu katika kila shughuli kanuni inakataa.

Nisinukuliwe vibaya wkwamba hakuna uwezekano kabisa wa mtu kujishirikisha katika shughuli zaidi ya moja,lakini kwa hatua za awali ni vema sana kukazana na kitu kimoja ambacho mafanikio yake yatazaa vitu vingine bila kupitia faida itakayozalishwa bila kuathiri mwenendo wa biashara yako mama.

Mara nyingi nimesema nguvu ya ujumbe wangu kwa binadamu wenzangu ni kuwashirikisha yale magumu na makosa niliyopitia katika maisha yangu ili wasirudie kufanya makosa yale yale tuliotangulia ili kuifanya safari yao ya mafanikio iwe fupi. Kama mambo haya ningefundishwa shuleni na ningeyajua katika hatua ya ujana wangu, basi leo ningekuwa nira zaidi. Namshukuru Mungu kwa kunipa nafasi ya kubadilisha changamoto na makosa niliyopitia maishani kuwa fursa ya kufundisha na kugusa maisha ya binadamu wenzangu.

Previous
Previous

Kuanzia Ulipo: Njia Kuelekea Kuishi Ndoto Zako.

Next
Next

“Anza Safari: Kuishi Kusudi La Kuwepo Kwako Duniani”