Jifunze Kupitia Makosa.

Makosa ni mwalimu muhimu katika maisha.

Kwa nini watu wengine wananufaika na hali ya kukosea na wengine wanapoteza kabisa mwelekeo wa maisha pale wanapofikia katika hali ya kukosea? Nini kinachofanya watu hao wawe tofauti? Kinachotofautisha watu hao wawili ni namna tofauti katika mitazamo yao,mmoja anaichukulia kama fursa na mwingine anaona kama kukosea ndio mwisho wa kila kitu. Ingawa watu wazima wengi wanachukulia kukosea kama njia ya kumsaidia mtu kukua na kupata uzoefu katika maeneo mengi ya maisha; kinyume chake watu wengi hasa vijana wadogo hawapendi kukosea na hivyo hukatishwa tamaa pale wanapojikuta wamekosea katika maisha. 

Kutegemeana na mtazamo wa mtu mmoja hadi mwingine,makosa yanaweza kutazamwa katika namna mbili; kwanza kama kipimo cha mtu kushindwa au mtazamo wa pili kama njia nzuri kukusaidia kuboresha na kurekebisha mahali ulipokosea.  Hakuna binadamu ambaye aliwahi kuishi au anaishi hata leo ambaye hana sifa ya kufanya makosa,kwa hiyo makosa ni hatua muhimu sana katika maendeleo ya mwanadamu yeyote na ama anayeishi au aliyewahi kuishi.

Mtu yeyote bila kujali hali,uwezo,mahali alipo,umri au cheo chake wote wanayo sifa hii muhimu ya kukosea. Wafalme wanakosea,watoto na wakubwa wanakosea,matajiri wanakosea,maskini wanakosea,wazungu,waafrika,wahindi,waarabu wanakosea.  Hebu futuatilia historia ya watu waliofanikiwa sana katika maeneo mbalimbali ya maisha duniani utagundua kwamba pamoja na umaarufu wao pia wanaongoza kwa kukosea. Kuwa kiongozi katika eneo fulani hakumwondolei mtu sifa muhimu ya kibinadamu kukosea. 

Kukosea ni kitu cha lazima iwe mtu anataka au hataki,anajua au hata bila kujua lazima awe nayo sifa ya kukosea na kupitia wingi wa makosa anayofanya ndicho kipimo na kigezo cha hekima na uzoefu wa mtu katika maisha yake. Dunia tunayoishi imeumbwa ikiwa na mategemeo ya kukaliwa na watu wenye mapungufu mengi wanakosea kila kukicha na kwa maana hiyo mtu hapaswi kufika mahali kushindwa kufanya kitu kwa kusukumwa tu na hofu kwamba mbele inaonekana unaweza kukosea hapana.   

Kwa nini watu wengine wananufaika na hali ya kukosea na wengine wanapoteza kabisa mwelekeo wa maisha pale wanapofikia katika hali ya kukosea? Kinachotofautisha watu hao wawili ni namna tofauti katika mitazamo yao,mmoja anaichukia kama fursa na mwingine anaona kama kukosea ndio mwisho wa kila kitu. Hapa kuna mambo machache muhimu ambayo ningependa tushirikiane katika makala yetu hii fupi ya leo ambayo naamini yatakusaidia sana katika safari yako ya kutafuta mafanikio maishani mwako kwenye eneo ambalo umepkwa mafuta kutumika.

1. UZOEFU NI TUNDA LA MAKOSA.

Uzoefu ni kitu ambacho kila mtu anatamani kuwa nacho lakini ukweli ni kwamba uzoefu kamili huundwa na vitu viwili:mchanganyiko wa mambo ambayo umefanya kwa mafanikio katika maisha ukichanganya na makosa mengi ambayo umefanya katika maisha yako. Makosa ni kiungo muhimu sana katika mchango wa kutengeneza uzoefu wa aina yoyote katika maisha,kwa hiyo hakuna uzoefu bila kukosea.Ukikutana na mtu anayejitambulisha kuwa anao uzoefu wa kufanikiwa tu katika maisha mtu huyo bado hana uzoefu maanake hajakosea. 

2. HUTUSAIDIA KUKUA

Usiogope kukosea kwa sababu makosa yanatusaidia sana kukua.Bila kukosea tungebaki tunajua yale tunayojua tu.Kufanya makosa kunafungua macho yetu kwa kutupa nafasi muhimu ya kupata maarifa mapya ambayo pengine hata huyajui pale tunapotafuta kurekebisha makosa yetu. 

3. HUONGEZA HAMU YA KUFANYA VIZURI

Kwa mtu anayechukulia makosa kama fursa huongeza kiwango cha hamu ya kutaka kufanya sahihi na hivyo kuchochea kutafuta maarifa kurekebisha makosa mtu aliyofanya. Bila kukosea mtu hangeweza wakati mwingine kupata maarifa mapya.

4. MAKOSA YANATUMIKA KAMA TAHADHARI

Ukifanya makosa yanayosabisha matokeo mabaya au kwa watu wanaokuzunguka,hutafanya tena kosa hilo tena kwa sababu utakuwa na tahadhari kwa kuwa umekwisha pata namna bora zaidi ya kufanya bila kukosea tena.

5. HUMREJESHA MTU KWENYE UHALISIA

Wakati mwingine mtu anapofanikiwa sana katika kila jambo analofanya hujaribiwa kufikiri kuwa kukosea haiwezekani.kujivuna na pia kukosa ukweli halisi wa maisha. Kukosea kutakusaidia kuongeza unyenyekevu uhalisia kuwa wewe ni mwanadamu tu. Watu waliofanikiwa sana katika mahusiano na watu wengine ni wale waliokosea sana pia katika maisha yao. Tofauti ya watu hao na wengine ni namna wanavyopokea na kukiri makosa pale wanapobaini au kupata watu wa kuwasaidia kuona kosa.

6. HUTUONGEZEA HEKIMA.

Kila kosa unalofanya huja na somo fulani,na unapojifunza kutokana na makosa hayo basi hukusaidia kupata hekima. Franker aliwahi kusema nanukuu “Makosa ni sehemu ya ubinadamu. Tambua makosa yako jinsi yalivyo na kupata masomo muhimu ambayo yanaweza kupatikana kupitia nyakati ngumu,ambazo wengine wanaweza kujifunza kwazo”

7. HUTUFUNDISHA KUSAMEHE NA KUCHILIA

Kitu kimojawapo kikubwa cha kujifunza kutokana na makosa ni kwamba yanatufundisha kujisamehe na kusamehe watu wengine pia. Watu wengi walio wepesi kujisamehe ni wepesi pia kusamehe watu wengine waliowakosea. Makosa yanatusaidia kuachilia kwa sababu usipoachilia hutaweza kusamehe na hivyo hutaweza kupona maana kuachilia ni kwa faida yako.

Kuwasamehe watu wengine kunategemea sana kumbukumbu ya wingi wa makosa ambayo tumefanyia watu wengine nao wakatusamehe. Bila kufanya makosa ni rahisi sana kuwa katika nafasi ya kujihesabia haki kana kwamba sisi hatukosei. Kukosea ni muhimu sana katika maisha ya mwanadamu kwa sababu kadri mtu anavyokosea ndivyo anavyokuwa na uwezo wa kurekebisha na kuwa bora zaidi katika maeneo ambayo amefanya makosa. Leo amekosea na kujipa nafasi ya kutafakari kwa nini amefanya kosa hilo na ni nini anaweza kufanya kuweza kuepuka kufanya kosa kama hilo siku za usoni? 

Kabla hujasahau kabisa habari za mwaka jana hebu nikuombe tu kwamba kumbuka ni maeneo gani mwaka jana moyo wako unakushuhudia kuwa ulikosea na kujikuta umekwama mahali fulani,halafu tafuta ni somo gani muhimu unaweza kujifunza kutokana na makosa hayo kisha jipe nafasi ya kujiuliza nini unaweza kufanya kurekebisha na kufanya vizuri zaidi? Nimalizie tu kwa kusema kuwa watu wengi watakukatisha tamaa kila unapokosea,mimi nataka nikwambie tu kwamba kosea mara nyingi kadri utakavyoweza kwa sababu dunia ya watu wasiokosea bado haijaumbwa. 

Kama unadhani kuna kitu cha kukusaidia umepata kutoka katika makala hii fupi tafadhali tunakuomba uache ujumbe hapo chini kwa ajili ya kuwatia moyo wasomaji wenzako wanaotembelea mtandao huu. Na kama ungependa kuingia kwa undani katika mada hizi kwa maswali au kujifunza zaidi usisite kuwasiliana nasi kwa kutuma ujumbe mfupi wa simu,kupiga au whatsapp kupitia simu hapo chini. 

Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale

 Simu/WhatsApp: +255784503076  

Email: maishanifursa2017@gmail.com

Previous
Previous

Ninalotaka Silifanyi, Nafanya Nisilotaka!!!

Next
Next

“Nguvu Ya Imani Katika Kila Unalofanya”